Cassian Njowoka akikabidhi msaada wa Kompyuta kwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Nyasa, Francis Homanga kwa ajili ya matumizi ya chama hicho wilayani humo. |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
VIONGOZI na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya
Nyasa mkoani Ruvuma, wametakiwa kuacha kutengeneza majungu na mifarakano ndani
ya chama hicho na kwamba endapo wataendekeza mambo hayo, huenda wakasababisha malumbano
na kukigawa chama.
Cassian Njowoka. |
Aidha viongozi wa CCM wameshauriwa kutembelea wananchi wao
katika maeneo yao mara kwa mara, ili kukifanya chama kiweze kuwa endelevu
katika kupigania haki na maendeleo husika katika jamii.
Hayo yalisemwa na Cassian Njowoka ambaye ni Kamanda wa Umoja
wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa, alipokuwa akizungumza
na wananchi wa kata ya Kingirikiti wilayani humo katika hafla fupi ya kukabidhi
msaada wa vifaa vya chama hicho.
Njowoka alikabidhi msaada wa mashine ya kisasa ya fotokopi,
printa, kompyuta mbili pamoja na katoni mbili za rimu za karatasi kwa ajili ya
kuchapia barua za aina mbalimbali.
Alisema kuwa vifaa hivyo vitaweza pia kukisaidia chama hicho,
kuanzisha mradi wake utakaosaidia kujipatia fedha za kuendeshea chama na
kuepukana na mtindo wa kuwa omba omba.
Pamoja na mambo mengine Kamanda huyo wa UVCCM ameweza kulifanyia
matengenezo gari la Chama cha mapinduzi wilayani humo, ambalo liliharibika kwa
muda mrefu lilikuwa halifanyi kazi, matengenezo ambayo yamegharimu fedha za
kitanzania shilingi milioni 2.3.
Vilevile kwa upande wake akipokea msaada huo, Mwenyekiti wa
CCM wilaya ya Nyasa Francis Homanga alisema kuwa wanamshukuru kwa mwenendo wake
mzuri wa kukisaidia chama mara kwa mara, huku akimtaka moyo huo alionao
aendelee nao kwa manufaa ya kuisaidia jamii.
“Nampongeza Njowoka kwa jitihada hizi anazozifanya kwa
uzalendo wake wa kuchangia maendeleo ya wilaya hii, mambo mengi ya kimaendeleo
pale tunapomuomba msaada amekuwa mwepesi kutusaidia”, alisema Homanga.
Homanga alibainisha kuwa Njowoka ameweza kuchangia mifuko ya
saruji katika ujenzi wa zahanati, miundombinu ya maji, shule za msingi na
sekondari pamoja na ufungaji wa mfumo wa umeme jua katika maeneo ya kutolea
huduma za afya vijijini.
No comments:
Post a Comment