Na Julius Konala,
Songea.
KATIKA kuhakikisha kwamba agizo la serikali linatekelezwa juu
ya ujenzi wa vyoo bora vya kisasa katika shule za msingi na sekondari hapa
nchini, diwani wa kata ya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Issack
Lutengano kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amechangia kiasi cha
shilingi milioni 1,000,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa choo cha
walimu, shule ya msingi Msamala iliyopo mjini hapa.
Mchango huo ulikabidhiwa juzi kwa Mwalimu mkuu wa shule hiyo,
Mariam Kinyunyu baada ya kutoa ombi hilo kwa diwani huyo ambaye alikuwa mgeni
rasmi katika mahafali ya 34 ya shule hiyo, ambapo alisema kuwa katika hatua ya
kwanza ya ujenzi wa choo hicho tayari zimetumika shilingi milioni mbili huku makadirio
yakiwa ni shilingi milioni tatu mpaka kukamilika kwake.
Akizungumza katika mahafali hayo diwani Issack alisema kuwa
atahakikisha anashirikiana na halmashauri hiyo, wazazi na wananchi wa kata hiyo
katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili shule yake ikiwemo pia ujenzi
wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.
Vilevile amewataka wahitimu hao, kujitunza kipindi hiki wanachosubiri
matokeo ya mitihani yao na kwamba ametoa onyo kali kwa wale wote wenye tabia ya
kuwapa ujauzito wanafunzi, waache mara moja vitendo hivyo huku akiahidi
kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayehusika kufanya hivyo.
“Natoa onyo kali kwa mzazi yeyote atakayegundulika
kutompeleka mtoto wake shule wakati akijua mwanaye amefaulu na kukimbilia kumuozesha,
katika hili sitakuwa na huruma nitawafikisha kwenye vyombo vya kisheria”,
alisisitiza Issack.
Awali Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Mariam
alimwambia diwani huyo kuwa shule ya msingi Msamala inakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo utoro wa wanafunzi, wizi wa vifaa vya walimu, kung’oa miti
iliyopandwa eneo la shule, ukosefu wa ofisi ya walimu, upungufu wa vyumba vya
madarasa na matundu ya vyoo.
Kufuatia hali hiyo Kaimu Ofisa elimu wa Manispaa ya Songea
Castor Mbano, amewataka wazazi kushirikiana na walimu katika kudhibiti utoro na
kuondoa changamoto hizo ikiwemo kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi na
atakayekaidi achukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
No comments:
Post a Comment