Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa Watendaji ambao wamepewa dhamana ya kukusanya
mapato katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, endapo kama
watakosa uaminifu katika kutekeleza ipasavyo majukumu waliyopewa, wajiandae
kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi.
Aidha kwa wale ambao wanatabia ya kuwa wadanganyifu na
kushirikiana na wafanyabiashara wajanja kutorosha mapato ya halmashauri hiyo,
kwa lengo la kujinufaisha matumbo yao nao wanatafutiwa mwarobaini wao.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gumbo
Samanditu alisema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na Madiwani
wake kwenye ukumbi wa umati uliopo mjini hapa, juu ya uwekaji mikakati thabiti
ya ukusanyaji mapato kwa halmashauri hiyo.
“Ndugu zangu Madiwani, nataka niwaambie kwamba watendaji wa
namna hii tukiwabaini mimi nitawatumbua tu, sina mchezo katika hili na sihitaji
kufanya mzaha wa aina yoyote ile katika majukumu yetu tuliyopewa na serikali”,
alisema Samanditu.
Samanditu alisisitiza kuwa, ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea
kuna kila sababu sasa kwa watumishi waliopewa kazi ya kutekeleza jukumu hilo
kuwa waaminifu kwa kujenga ushirikiano wa pamoja wakati wa utekelezaji wa jambo
hilo, kuanzia ngazi ya vijiji hadi kata.
“Kwenye suala la udhibiti tushirikiane kwa pamoja kwenye
maeneo yale ya vijiji hadi kata, hatuhitaji kusikia mtu anakwepa kulipa ushuru
tukimkamata tutampiga faini na Mahakamani atapelekwa ili hatua za kisheria
ziweze kufuata mkondo wake”, alisema.
Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano ambayo inaongozwa na
Rais Dkt. John Magufuli, haipendi kuona mambo yanakwenda hovyo na endapo kama
kutakuwa na kero yoyote ofisi yake ipo wazi, apewe taarifa haraka ili aweze
kuchukua hatua.
No comments:
Post a Comment