Felix Mkuruha mkazi wa mtaa wa Ruhuwiko shuleni Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, akionesha shamba lake alilozalisha vitunguu baada ya kuwezeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani humo. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
RUZUKU ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF)
inayotolewa kwa kaya maskini katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imeweza
kubadilisha maisha kwa baadhi ya kaya hizo na kuweza kuendesha maisha yao bila utegemezi.
Katika ziara ya kutembelea na kukagua kaya maskini ambayo
ilihusisha maafisa wa mfuko huo na waandishi wa habari katika kata ya Mjimwema
mjini Songea, baadhi ya wananchi waliopata ruzuku hiyo walisema kuwa maisha yao
yamebadilika na kwamba hivi sasa, wamekuwa wakiendesha miradi ya aina
mbalimbali ambayo imekuwa ikiwaingizia kipato.
Hawa Hassan (60) mkazi wa mtaa wa Kijiweni kata ya Mjimwema
alisema kuwa kabla ya kuwezeshwa na TASAF, alikuwa na hali mbaya kimaisha baada
ya kuachwa na mumewe kutokana na kuugua maradhi ya miguu lakini hivi sasa anao uwezo
wa kumudu gharama za maisha yake.
“TASAF walinipatia ruzuku ya shilingi 36,000 kila baada
ya miezi mitatu nilianzisha biashara ndogondogo ya kuuza mafuta ya kula na
nyanya na baadaye nikafanikiwa kuwa na mtaji wa shilingi laki moja, nilinunua
kuku wa mayai 74 ambao ni wa kienyeji na sasa naendelea kuwafuga na wananipatia
kipato cha kuendeshea maisha yangu”, alisema Hawa.
Hawa alisema pia anaouhakika wa maisha, hata kama serikali
itasimamisha ruzuku inayotolewa na Mfuko huo wa maendeleo ya jamii miradi yake
itaendelea vizuri na kwamba kuku wake wanataga mayai, ambayo huyauza na
kujipatia fedha taslimu za kuendeshea maisha yake.
Naye Katerina Kayombo (70) mkazi wa mtaa wa Mjimwema alisema
tangu alipoanza kupata ruzuku kutoka kwenye mfuko huo, ameachana na tabia ya
kuwa ombaomba baada ya kuanzisha bustani ya mbogamboga ambayo humuingizia
kipato.
Wananchi wengine waliohojiwa walisema kuwa kutokana na
kuwezeshwa na TASAF hivi sasa wanauhakika hata wa kula milo mitatu kwa siku,
tofauti na hapo awali walikuwa na maisha magumu ambapo wanajishughulisha na biashara
ndogo ndogo zinazowafanya waweze kupata fedha za kuendeshea maisha yao ya kila
siku.
Wengine walisema wameweza kujenga nyumba za kuishi ambazo
zimeezekwa bati ambapo hapo awali walikuwa wakiishi kwenye vibanda vibovu ambavyo
vilikuwa vimeezekwa kwa maturubai, ambapo nyakati za masika vibanda hivyo
vilikuwa vikivuja na kuwaletea adha kubwa.
Christopher Ngonyani ambaye ni afisa wa TASAF halmshauri ya Manispaa
ya Songea, alisema kuwa ameendelea kupokea fedha kwa ajili ya mpango wa
kunusuru kaya maskini, kupitia mradi huo awamu ya tatu ikiwa ni lengo la kupunguza
umaskini kwa watu wasiojiweza.
Ngonyani alibainisha mwezi Julai mwaka 2015 hadi Mei 2016
zaidi ya shilingi bilioni 1.628 zilipokelewa na zimeendelea kutolewa kwa
kaya maskini zilizopo kwenye Manispaa hiyo.
Alisema
Katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2015/2016 kazi mbalimbali zimeendelea
kufanyika ambazo ni kulipa kaya maskini 7,828 kati ya lengo la kaya 7,915
zilizopo kwenye mpango huo, ambapo kaya 88 hazikuweza kujitokeza wakati malipo hayo
yanafanyika na kwamba fedha zao zimerudishwa makao makuu ya mfuko huo, Jijini
Dar es Salaam kulingana na taratibu husika.
Ngonyani
alisema kuwa ili kuweza kufikia malengo ya mfuko huo wameweza kutoa mafunzo pia
kwa watendaji wa kata, wauguzi, walimu shule za msingi na sekondari kwa kuwajengea
uelewa watumishi hao ili wasaidie katika kuondoa umaskini hasa katika kufuatilia
masharti ya elimu na afya.
Pia uchunguzi
umebaini kuwa mpango huo wa TASAF katika kunusuru kaya maskini umeleta
mafanikio makubwa ikiwemo kuimarika kwa mahudhurio ya watoto shule za msingi na
sekondari, kuongezeka kwa mahudhurio ya watoto wenye umri wa chini ya miaka
mitano kwenda Kliniki na wanufaika wengi kuanza kujiunga na Mfuko wa Afya ya
Jamii (CHF).
No comments:
Post a Comment