Mbinga.
HATIMAYE zoezi la uhamasishaji upimaji ardhi ya wananchi
katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limepokelewa kwa mikono
miwili katika vijiji, kata na miji midogo iliyopo wilayani humo ambapo wakazi waliopo
katika maeneo husika kwa nyakati tofauti wamefurahia mpango huo na kuutaka
uongozi wa wilaya hiyo kuanza mara moja kazi ya upimaji wa ardhi yao, ili waweze
kunufaika nayo katika kusukuma mbele maendeleo yao.
Mafanikio hayo yametokana na elimu iliyokuwa ikitolewa na
timu ya wataalamu ambayo iliundwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya
hiyo, Gombo Samandito ambapo ilikuwa ikipita katika kila kijiji, kata na miji
midogo iliyopo wilayani humo kuhamasisha juu ya umuhimu wa upimaji ardhi kisheria
na kuwafanya wakazi waliopo katika maeneo husika wasiweze kujenga kiholela.
Zoezi hilo la uhamasishaji limetekelezwa kwa siku saba,
ambapo lilianza rasmi Agosti 15 mpaka 21 mwaka huu likiongozwa na Mkurugenzi
huyo, ambapo imeelezwa kuwa hatua hiyo
itasaidia wananchi kumiliki ardhi yao kisheria sambamba na kupewa hati ambazo
watazitumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi, kwa kupata
mikopo kutoka taasisi za kifedha kama vile benki.
Jumla ya vijiji 118, kata 29 pamoja na miji minne ya Ruanda, Matiri,
Kigonsera na Maguu ndiyo ambayo inatarajiwa kupimwa wilayani Mbinga ili
wananchi hao waweze kunufaika na kwamba upimaji huo unatarajiwa kuanza kufanyika
wakati wowote kuanzia sasa, kufuatia zoezi hilo la utoaji elimu kwa wananchi
kukamilika taratibu zake.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali
yaliyokuwa yakitolewa elimu hiyo juu ya umuhimu wa upimaji huo, Mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya wilaya hiyo, Samandito alisema kuwa utekelezaji huo ni agizo
la Rais Dkt. John Magufuli ambapo amezitaka halmashauri zote za wilaya, miji na
manispaa hapa nchini kuhakikisha kwamba zinapima ardhi yake ili kuweza
kuondoa migogoro inayoendelea kufukuta katika jamii na wamiliki husika waweze
kulipa kodi kwa urahisi kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya wananchi.
Alisema kuwa gharama za upimaji wa ardhi itakuwa shilingi
100,000 kwa ekari moja maeneo ya vijijini na kwamba katika miji midogo
itakuwa shilingi 200,000 kwa ekari moja badala ya shilingi 300,000
ilivyokuwa hapo awali katika kipindi cha miaka ya nyuma, huku kodi
ya ardhi kwa mwaka mmiliki halali atapaswa kulipia shilingi mia nne kwa
ekari moja.
Naye mthamini wa ardhi katika halmashauri hiyo, Gabriel
Kameka aliwaeleza waandishi wa habari kuwa endapo watafanikiwa kupima ardhi yote
ya wilaya ya Mbinga katika miji midogo na wilaya kwa ujumla, wataweza kukusanya
kodi shilingi bilioni 6.7 kwa mwaka ambayo itatokana na heka 67,000
zitakazokuwa zimepimwa.
“Hili suala ni lazima tulivalie njuga sisi sote, tujenge
ushirikiano tuweze kufanikiwa, kama hatutakuwa pamoja ni sawa na kutwanga maji
kwenye kinu na mafanikio tunayoyatarajia hayatakuwepo”, alisema Kameka.
Alifafanua kuwa siku zote ardhi iliyopimwa mwananchi
ananufaika nayo kwa njia mbalimbali ikiwemo kwanza ni dhamana kwake, kufuatia
hati aliyonayo inamfanya aweze kukopa kwenye taasisi za kifedha na kumwezesha
kufanya shughuli zake za maendeleo.
Pia aliongeza kuwa zoezi hilo litaenda sambamba kwa serikali
kutenga maeneo muhimu kwa ajili ya shughuli za kijamii kama vile shule, viwanja
vya michezo, huduma za afya, barabara, miundombinu ya maji na maeneo ya
kuzikia.
Evalina Ndimbo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lukiti kata ya
Linda wilayani hapa alisema kuwa mpango huo endapo utafanikiwa utasaidia kuepusha
migogoro mingi ya ardhi iliyopo katika vijiji, kata na miji huku wananchi
waliopo katika maeneo husika wakizingatia kufuata sheria na taratibu
zilizowekwa.
Kwa ujumla Wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga,
walisema kuwa wamefurahishwa na mpango huo wa kimaendeleo unaotekelezwa na
wataalamu wake, hivyo waliahidi kujenga ushirikiano wakati zoezi hilo la
upimaji mara litakapoanza ili liweze kuleta ufanisi mzuri katika jamii.
No comments:
Post a Comment