Juma Homera Mkuu wa wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, akisisitiza jambo katika baadhi ya vikao vyake vya kikazi wilayani humo. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma imewaagiza Madiwani
wake, kuhakikisha kwamba wanajenga ushirikiano wa pamoja kubaini wanafunzi hewa
katika shule zake za msingi ili kuweza kupambana na walimu wasiokuwa waaminifu
na wenye mpango wa kuiibia fedha zake, ambazo hutolewa kila baada ya miezi
mitatu kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi mashuleni.
Aidha katika kuhakikisha kwamba jambo hilo linafanikiwa,
imeahidi kuunda tume itakayofuatilia utekelezaji huo kwa kufanya uhakiki kwa shule
zote za msingi wilayani humo ili kujiridhisha uhalali wa matumizi ya fedha
hizo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera alisema hayo wakati
alipokuwa akitoa salamu za serikali kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi
katika ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya Mlingoti mjini hapa.
Homera alifafanua kwamba serikali wilayani hapa inazo taarifa
kwamba, wapo walimu ambao sio waaminifu wamekuwa wakipeleka orodha ya majina ya
watoto wasiolingana na idadi halisi ya wanaosoma katika shule husika, ili
waweze kujipatia fedha hizo za ziada kwa ajili ya kujinufaisha matumbo yao.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa wilaya aliwataka madiwani
kwenda kuhakiki shule zilizopo kwenye maeneo yao, ili wajiridhishe juu ya madai
hayo yaliyopo ambayo husababisha fedha za serikali kupotea pasipo kufanya kazi
iliyolengwa.
Takwimu kutoka ofisi za idara ya elimu msingi wilayani
Tunduru zinaeleza kuwa wilaya hiyo ina jumla ya shule 150 za msingi, ikiwemo ndani
ya shule hizo moja inamilikiwa na mtu binafsi.
No comments:
Post a Comment