Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA kuhakikisha kwamba uchumi wa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma unakuwa endelevu, kampuni ya Tutunze Kahawa Limited (TKL) iliyopo
wilayani humo imeanzisha kitalu mama cha kuzalishia miche bora ya kahawa na
kwamba mara baada ya uzalishaji huo kufanyika, miche hiyo hugawiwa bure katika
vikundi vya wakulima.
Ukuzaji wa miche hiyo ya kahawa ni ile ya kisasa maarufu kwa
jina la Vikonyo ambayo inastahimili magonjwa mbalimbali, yakiwemo yale ya kutu
ya majani na vidung’ata.
Thomas Ngapomba ambaye ni Meneja masoko wa Kampuni hiyo
alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake, ambao walitembelea makao makuu ya ofisi hizo zilizopo mjini hapa kwa
lengo la kujionea maendeleo wanayoyafanya katika kukuza kilimo cha zao hilo
wilayani humo.
Ngapomba alifafanua kuwa kwa mwaka wamekuwa wakizalisha zaidi
ya miche 100,000 ambayo husambazwa kwa wakulima waliopo katika vikundi, ambavyo
vimesajiliwa kisheria na wakati huo wanajishughulisha na uzalishaji wa kahawa
bora.
“Mpaka sasa tuna jumla ya vikundi 165 ambavyo hunufaika na
mpango huu tuliojiwekea, tumekuwa hasa tukisaidia vikundi vile ambavyo havina
uwezo wa kuendesha shughuli zao za kilimo cha kahawa ndani ya kikundi husika”,
alisema Ngapomba.
Kadhalika aliongeza kuwa TKL imekuwa ikitoa mikopo ya
pembejeo za kilimo kwa masharti nafuu kwenda kwa wakulima hao, ili waweze
kuboresha mazao yao shambani.
Alisema kuwa katika msimu wa mwaka 2015/2016 wameweza kutoa
mkopo wenye thamani ya shilingi milioni 149,356,000 kwa wakulima 500.
No comments:
Post a Comment