Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MVUTANO mkali umetokea katika kikao cha baraza la Madiwani
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kufuatia baadhi ya madiwani kupinga hoja
inayohusu kutumika kwa stendi ya zamani iliyopo mjini hapa kwa mabasi
yanayosafirisha abiria kwenda nje ya mkoa huo, wakitaka mabasi hayo yaanze
safari zake katika kituo kipya cha Msamala kilichopo mbali na mji huo.
Kufuatia hali hiyo lilibuka kundi la Wananchi ambao nao
walihudhuria kusikiliza mkutano huo na kuanza ghafla kuzomea madiwani waliokuwa
wakipinga hoja hiyo, jambo ambalo lilihatarisha kuvunjika kwa amani ndani ya
kikao hicho kilichoketi juzi kwenye ukumbi wa Manispaa hiyo mjini hapa.
Aidha katika baraza hilo Meya wa Manispaa hiyo Abdul
Mshaweji, Mbunge wa Songea mjini, Leonidas Gama na madiwani wengi waliokuwa
wakiunga mkono hoja hiyo walionekana kushangiliwa na wananchi hao huku wengine
wakipaza sauti zao wakisema, wanataka mabasi hayo ya abiria yaanze safari zake katika
stendi hiyo ya zamani na sio vinginevyo.
Wananchi hao walisikika wakieleza kuwa wamekuwa wakipata
shida kwa muda mrefu kwenda kupanda mabasi katika stendi hiyo ya Msamala ambayo
ipo mbali na mji huo, jambo ambalo hulazimika kutumia fedha nyingi kukodi taxi
mpaka kufika huko Msamala.
Baada ya kuonekana hali inazidi kuwa mbaya ndipo Mkuu wa
wilaya ya Songea Palolet Mgema, alichukua jukumu la kuingilia kati kunusuru
hali hiyo ili machafuko yasiweze kutokea baada ya kuonekana dalili kwamba kuna
baadhi ya kikundi cha madiwani ndani ya kikao hicho kutaka kuanza kuleta fujo.
“Ninaona mnataka kukiharibu kikao kwa hoja ambayo haina
nguvu, kama kuna agenda muhimu mnataka ijadiliwe fuateni kanuni na taratibu za
kuwasilisha hoja siyo kila mtu anasimama na kuzungumza bila utaratibu, mimi
nikiwa Mkuu wa wilaya sipo tayari kuona uvunjifu wa amani ukitokea sitamvumilia
mtu yeyote wala kikundi chochote humu ndani, ambacho kitasababisha uvunjifu wa
amani”, alisema Mgema.
Mkuu huyo wa wilaya, Mgema alisema iwapo kama diwani anahoja
muhimu binafsi ya kupinga suala hilo alipaswa kufuata utaratibu na kuiwasilisha
agenda hiyo mapema, kabla ya kikao hicho kuanza na sio kukurupuka na kuanza
kupinga wakati tayari lilikwisha pitishwa katika maamuzi husika.
Hali ya utulivu iliporejea Diwani wa kata ya Msamala kupitia
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Issack Lutengano, alipinga hoja ya
mabasi kuanza kupakia abiria stendi hiyo ya zamani huku akisema kwa jazba
kwamba Meya wa Manispaa hiyo, Mshaweji aache kuendesha baraza kwa kuendeshwa na
wapambe wachache.
Kauli hiyo ya Lutengano ilianza kuzua mvutano mkali kati yake
na Meya huyo ambaye licha ya kujitahidi kumwelekeza afuate kanuni za vikao,
hata hivyo hakutaka kumsikiliza badala yake alikuwa akiendelea kuongea kwa
jazba huku wananchi waliofika kusikiliza kikao hicho, wakianza kuwazomea tena
madiwani hao ambao walikuwa wakipinga hoja ya mabasi ya kusafirisha abiria
mjini hapa kuanza safari zake eneo la stendi hiyo ya zamani.
Naye Diwani wa kata ya Ruvuma, kupitia Chama Cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) Rashid Mososa alisema yeye haoni dhambi mabasi hayo
kuanza safari zake katika stendi ya zamani hadi stendi mpya ya Msamala na
kwamba aliwataka Madiwani wenzake kuwaonea huruma wananchi, ambao wanatoka
mbali hulazimika kutumia usafiri wa taxi kwa kukodi kwa gharama kubwa kwenda
kupanda mabasi katika stendi hiyo mpya ambayo ipo mbali na mji wa Songea.
Kwa upande wake naye Naibu Meya, Consolatha Kilowoko wa CCM
aliwataka madiwani wenzake kuwa na ubinadamu na kuacha kuwaumiza wananchi kwa kuendekeza
maslahi yao binafsi, badala ya kutetea wananchi wenye maisha magumu.
Hata hivyo Mbunge wa viti maalum wa Chama Cha Mapinduzi
Judith Mbogoro aliwataka madiwani hao kuunga mkono hoja ya mabasi kuanzia
stendi hiyo ya zamani, ili kuweza kuwasaidia hata wanawake wajawazito na watoto
wadogo waweze kupata huduma ya usafiri kwa ukaribu zaidi hoja ambayo baadaye
iliungwa mkono na wengi wao katika kikao hicho cha baraza la madiwani.
No comments:
Post a Comment