Wednesday, August 3, 2016

MBINGA WAHAMASISHWA KUJIUNGA NA MIFUKO YA AFYA YA JAMII



Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

MKURUGENZI mtendaji halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Gumbo Samanditu amewataka Madiwani, Watendaji wa vijiji na kata wilayani humo kuelimisha wananchi katika maeneo yao juu ya umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na ule wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kupata matibabu kwa urahisi.

Samanditu alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na Madiwani hao kwenye mafunzo ya siku moja, yaliyolenga kuwajengea uwezo katika kuibua vyanzo vipya vya mapato na ukusanyaji wa mapato ndani ya halmashauri hiyo.

Alisema kuwa kiasi cha shilingi 20,000 kwa mwanachama wa CHF na shilingi 76,800 ambacho mwanachama  wa NHIF anatakiwa kulipia kama mchango wa kupata matibabu kwa mwaka, sio kikubwa ikilinganishwa na gharama halisi ya matibabu anayotakiwa kulipa mgonjwa pale anapokwenda hospitali kwa ajili ya kupata huduma ya matibabu.

Alifafanua kuwa serikali inatambua umuhimu wa kuwajengea afya bora wananchi wake, ili waweze kufanya shughuli za kimaendeleo na kukuza uchumi wa taifa hili hivyo iliona ni vyema kuanzisha mpango huo wa matibabu ambao unamfanya mwananchi wa kawaida, kupata huduma husika kwa kipindi cha mwaka mzima.


Samanditu alibainisha kuwa hapo awali huduma hizo zilikuwa zikitolewa kwa watumishi wa serikali pekee, lakini hivi sasa zimeelekezwa hata kwa watu wengine wa kawaida kwa masharti nafuu ya kuwa mwanachama na kuchangia gharama kidogo kila mwaka.

Pia Madiwani hao amewataka kuhakikisha kwamba wanatoa elimu ya kutosha kwa wananchi wao, kwani mpango huo umesaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi hasa pale wanapougua na kukosa fedha za kugharamia matibabu.

“Nataka kuhakikisha wananchi wote wilaya ya Mbinga wanaingia katika mpango huu wa NHIF na CHF ili waweze kuwa na uhakika wa kupata huduma za tiba katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zetu”, alisisitiza.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii hapa wilayani Mbinga, Benedict Mkuwa aliwasisitiza Madiwani hao kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi wao, kuchangamkia fursa hiyo ili jamii iweze kuimarisha afya zao na hatimaye kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo.

Pamoja na mambo mengine, hadi sasa wilaya ya Mbinga haijafanya vyema katika mpango wa CHF na NHIF kwani ina watu zaidi ya milioni 1,376,891 kaya 303,071 na kwamba hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu idadi ya waliojiunga na mfuko huo ni watu 54,345 tu ambayo ni sawa na asilimia 17.93.

No comments: