Na Muhidin Amri,
Songea.
SHIRIKA la Bima Zanzibar limetoa mafunzo ya umuhimu wa watu
wenye ulemavu katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kujiunga na mifuko ya bima
za aina mbalimbali ili waweze kunufaika katika maisha yao.
Watu wenye ulemavu wapatao 100 kutoka wilayani humo
walipatiwa mafunzo hayo, ambayo yalifanyika kwenye ukumbi wa Chama cha akiba na
mikopo cha walimu uliopo mjini hapa.
Mafunzo hayo yalishirikisha watu wenye ulemavu wa aina
mbalimbali na walimu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wilayani hapa.
Akizungumza wakati alipokuwa akifungua mafunzo hayo Mkuu wa
wilaya ya Songea, Palolet Mgema amelipongeza shirika hilo kwa uamuzi wake wa kutoa
mafunzo hayo kwa watu hao wenye ulemavu huku akieleza kwamba ulemavu sio
ugonjwa kwa kuwa wenye ulemavu, wanaweza kusoma na kujifunza kama watu wengine
wasiokuwa na ulemavu.
“Natoa wito kwa jamii ni marufuku kuwaficha watoto wenye
ulemavu wa aina yeyote ile majumbani kwao, hawa wenzetu wanayo haki ya kupata
elimu kama wengine zipo shule za elimu maalum kwa ajili yao, tunahitaji
wapelekwe huko wakasome”, alisisitiza Mgema.
Alisema kuwa serikali inaowajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba
kundi hilo tete, linasaidiwa wakati wote kwa kila alichoeleza kuwa wapo wengine
wenye ulemavu ambao wanaweza kujishughulisha hata katika shughuli za kilimo na
kwamba aliahidi kuwa katika msimu ujao wa kilimo atahakikisha kwamba wanapewa
msaada wa pembejeo za kilimo ili waweze kuzalisha mazao yao shambani.
Pia alisema ofisi yake itaendelea kushirikiana na vyama vya watu
wenye ulemavu wilayani Songea, ikiwemo kuwasaidia kwa kuwapatia ardhi ili waweze
kuzalisha mazao ya aina mbalimbali.
Kwa upande wake akitoa mada ya elimu ya bima na faida zake
kwa watu wenye ulemavu ambazo hutolewa na shirika la bima Zanzibar, Meneja wa
shirika hilo Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Asha Alli amewataka walemavu hapa
nchini kujiunga na bima, ili waweze kuondokana na changamoto zinazowakabili
katika maisha yao kama vile matibabu pale wanapougua.
Asha amezitaja baadhi ya changamoto ambazo zinawapata watu
wenye ulemavu kama vile, hatari ya kugongwa na vyombo vya moto wanapokuwa
barabarani, kuibiwa na nyumba zao kuungua moto.
Kadhalika amezitaja bima ambazo hutolewa na shirika hilo kuwa
ni bima za magari ya aina zote, vyombo vya moto, ujenzi, bima za wizi, fedha
kwa ajili ya huduma mbalimbali, wafanyakazi na vyombo vya baharini.
Kwa mujibu wa Meneja huyo alisema kuwa mafunzo hayo
yamewajengea uwezo watu wenye ulemavu katika wilaya ya Songea, ambapo baadhi
yao wameamua kujiunga na bima mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo.
No comments:
Post a Comment