Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye. |
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
SERIKALI Wilayani Mbinga Mkoa wa
Ruvuma imewataka wakulima Wilayani humo kuachana na tabia ya kuuza mazao yao
yote, badala yake wajenge tabia ya kuweka akiba ya chakula ili waweze kuepukana
na njaa.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya
hiyo, Cosmas Nshenye alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake
ambao walimtembelea kwa lengo la kupata taarifa mbalimbali za maendeleo.
Nshenye alisema kuwa Serikali Wilayani
humo haitasita kuchukua hatua kali kwa wakulima wenye tabia ya kuuza mazao bila
kufuata taratibu na sheria zilizowekwa, ikiwemo kuwataka kuweka akiba ya
chakula ili kuwanusuru na balaa la njaa linaloweza kutokea hapo baadaye.
Alisema kuwa Serikali imekuwa
ikibebeshwa mzigo mkubwa pale inapotokea janga la njaa kwa kutafuta chakula kwa
ajili ya kuwasaidia watu waliokumbwa na tatizo hilo, licha ya wengi wao
walishazalisha chakula kwa wingi ambapo kutokana na kuwa na tamaa ya fedha
walijikuta wameuza chakula chote bila kukumbuka kuweka akiba kwa ajili ya
matumizi ya familia zao.
“Ndugu zangu nimelazimika kulisemea
hili kwa kuwa limekuwa ni tabia iliyozoeleka kwa baadhi ya wananchi
wamekuwa wanavuna mazao mengi ya chakula na biashara, lakini mwisho wa siku kutokana
na kuwa na tamaa ya fedha wanajikuta hawana hata chakula kwa ajili ya kulisha
familia zao sitaki hili lijitokeze katika Wilaya hii”, alisisitiza.
Mkuu huyo wa Wilaya Mbinga aliwataka
wananchi Wilayani humo kutoendekeza matukio ya sherehe za ngoma zisizokuwa na
msingi kwa kuwa zimekuwa zikitumia chakula kingi kwa wakati mmoja ili
kupatasifa ambazo hazina maana yeyote kwao na mwisho wake hujikuta wakiendelea kuwa
maskini.
Pamoja na mambo mengine aliongeza
kuwa msimu wa mavuno unakaribia hivyo watendaji wa Serikali waliopo vijijini
wanapaswa kuhakikisha kwamba wanawaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa
kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha katika familia zao.
No comments:
Post a Comment