Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI hapa nchini imeombwa
kuboresha sekta ya michezo hasa kwa mpira wa Pete, ili kuweza kuongeza na
kuimarisha vipaji vya wachezaji wa mpira huo na kulifanya Taifa liweze kusonga
mbele katika michezo.
Aidha Serikali kupitia Waziri wake wa
habari, utamaduni, sanaa na michezo Dkt. Harrison Mwakyembe imeombwa
kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa michezo katika Shule za msingi na sekondari
ili kuweza kuleta mabadiliko yenye tija.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na
Walimu wa Shule za msingi na Sekondari ambao walishiriki wa mafunzo ya siku
tatu, ya maboresho ya sheria mpya za mpira wa pete, yaliyofanyika kwenye ukumbi
wa Shule ya sekondari Mbinga iliyopo hapa Mkoani Ruvuma.
Walisema kuwa katika kuimarisha sekta
ya michezo ni vyema sasa kuandaa timu za michezo katika mfumo wa Academy, ambao
muda wote watoto shuleni wataweza kujifunza jambo ambalo litasaidia hata kuweza
kukuza vipaji na viwango vya uchezaji wa michezo hususan kwa mpira wa pete na
kuweza kufika mbali zaidi.
“Serikali yenyewe imekuwa ikitumia
Umoja wa Michezo Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na ule wa Shule za
Sekondari Tanzania (UMISSETA) kama ndiyo chuo cha mafunzo ya michezo, kitu
ambacho sisi tunaweza tukasema mfumo huu sio mzuri umekuwa kama vile mabonanza
na sio mashindano, kwa sababu huwezi kumuandaa mtoto shuleni kwa siku tano au
kumi akawa imara katika michezo”, walisema.
Gideon Albert ambaye ni mmoja kati ya
walimu walioshiriki mafunzo hayo kutoka Wilaya ya Mbinga Mkoani hapa alipohojiwa
na waandishi wa habari alisisitiza kuwa ni lazima sasa tunapaswa kuwa na
falsafa tofauti ya uchezaji mpira wa pete, huku akieleza kuwa wenzetu katika
nchi ya Uganda wanaamini kwamba Fast Possesion ndiyo mbinu pekee ya kuweza
kuboresha na kupata ushindi.
Albert aliongeza kuwa sisi Watanzania
bado hatujawa na falsafa yoyote ya kukuza vipaji vya mchezo wa mpira huo na
kwamba kila mmoja amekuwa na mifumo yake ambayo mwisho wa siku imekuwa
ikiturudisha nyuma na kutufanya tushindwe kusonga mbele.
Naye Regina Ngahi ambaye ni mwalimu
wa kutoka katika Manispaa ya Songea Mkoani humo alieleza kuwa mafunzo hayo ya
makocha na waamuzi wa mpira huo wa Pete, wamefurahi kupata ujuzi wa mabadiliko
ya sheria mpya zilizowekwa katika mchezo huo ambapo awali kutokana na kutoelewa
walikuwa wakilazimika kutumia sheria za zamani ambazo zilikuwa zikiwarudisha
nyuma kimchezo.
“Tumepata haya mafunzo inabidi sasa
tukayatendee kazi kwa wanafunzi wetu wa Shule za msingi na sekondari na hata
timu za mitaani katika maeneo ya kata zetu tunazoishi ili kuweza kuinua viwango
vya michezo hapa nchini”, alisema Ngahi.
Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo
wanapata cheti ambacho kinawathibitisha kwamba wao watakuwa wakufunzi, waamuzi
au makocha watakaoweza kuongoza timu ili hapo baadaye waweze kuunda timu moja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama
cha Mpira wa Pete Tanzania (CHANETA) Mkoani Ruvuma, Janeth Duga alisema kuwa
hapo awali sheria za mpira huo zilikuwa 21 lakini hivi sasa zipo 15 tu na
kwamba wameandaa mafunzo hayo kwa ajili ya walimu hao ili kuweza kuwapatia
ujuzi watakaoweza kwenda kuutumia kabla ya mashindano ya UMITASHUMTA na
UMISSETA hayajaanza ili waweze kupata na kutimia sheria hizo mpya.
Janeth alisema kuwa baada ya kumaliza
mafunzo walimu watarudi mashuleni na kwenda kuendesha mashindano hayo na
kuandaa timu husika ambazo zitakutana makao makuu ya Mkoa huo kwa lengo la
kutafuta timu ya Mkoa ambayo itawakilisha umoja huo wa michezo kwa shule za
msingi na sekondari Mkoani humo.
“Mashindano haya rasmi yataanza mwezi
wa tano mwaka huu yataendeshwa kwa muda wa wiki moja pale chuo cha ualimu
Matogoro Songea na baadaye wale washindi watachaguliwa kwenda Mwanza
kuwakilisha wenzao kwenye haya mashindano”, alisema Janeth.
Hata hivyo mafunzo hayo
yameshirikisha baadhi ya walimu wa kutoka Shule za msingi na sekondari katika
Wilaya ya Mbinga, Nyasa, Tunduru, Namtumbo, Madaba, Mbinga mji na Manispaa ya
Songea Mkoani Ruvuma ambapo walimu wengi walikuwa hawajui kwamba sheria za
mpira huu wa pete zimebadilika kutokana na kuwa na mazoea ya kutumia sheria za
zamani.
No comments:
Post a Comment