Na Mwandishi wetu,
Songea.
WAJASIRIAMALI wadogo 380 kutoka
vikundi 67 vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, wamepata
mafunzo juu ya mbinu za uwekezaji katika viwanda vidogo.
Mafunzo hayo ambayo yamefanyika
kwenye ukumbi wa Songea Klabu uliopo mjini hapa, yaliratibiwa na idara ya
Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo na kufundishwa na watalaam mbalimbali
wa taasisi na asasi za kifedha.
Akisoma taarifa ya vikundi hivyo Mkuu
wa idara hiyo, Naftari Saioloyi alisema kuwa Manispaa ya Songea imekuwa na
utaratibu wa kukopesha vikundi vya wanawake na vijana kutoka katika mapato yake
ya ndani.
Saioloyi alieleza kwamba katika
kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya vikundi 102 vilikopeshwa
Shilingi milioni 116 kati ya hizo, vikundi 87 vya wanawake vilikopeshwa zaidi
ya Shilingi milioni 101 na vikundi vya vijana 15 vilikopeshwa Shilingi milioni
14.9.
“Mikopo hii ililenga katika kila
kikundi kuendeleza miradi ambayo ilianzishwa, leo hii Manispaa imeona ni vyema
viongozi wa wanavikundi kukutana na wataalam kutoka taasisi za Serikali za
SIDO, VETA, TICCIA ili wapate mafunzo na kuweza kupanua wigo wao wa
uwekezaji’’, alisema Saioloyi.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga
kuviwezesha vikundi hivyo kutafakari namna ya kufanya shughuli zao kulingana na
maeneo wanayotoka, rasilimali walizonazo na upatikanaji wa soko kwa mazao
watakayozalisha.
Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo
hayo Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni
muhimu hasa katika kutekeleza kauli mbiu ya Serikali inayolenga Tanzania ya
viwanda kwa kila mkoa kuwa na viwanda 100.
Mgema alisema wajasirimali wadogo
watakapofanikisha kwenye uwekezaji hata kama ni wa kiwanda kidogo watakuwa
wamefikia kwenye malengo ya Taifa ya viwanda.
“Hakuna aliyezaliwa akaanza kutembea
bali huanzia na kutambaa, kusimama halafu kutembea, kiwanda kidogo kinaanza na
mtaji mdogo anzeni sasa ili baadaye mfikie hatua ya kufanya mabadiliko”,
alisema Mgema.
Mafunzo hayo ya mbinu za uwekezaji
katika viwanda vidogo yametolewa pia na taasisi za kifedha kutoka benki ya NMB,
CRDB na POSTA.
No comments:
Post a Comment