Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Na Mwandishi wetu,
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaja Mikoa ya Tabora, Geita,
Mtwara na Shinyanga kuwa ndiyo inayoongoza kwa utoro wa wanafunzi wa Sekondari hapa nchini.
Majaliwa ameitaja pia Mikoa ya Rukwa, Geita, Tabora, Singida
na Simiyu kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa shule za Msingi.
Alisema hayo leo Aprili 2 mwaka huu, wakati wa uzinduzi Mbio
za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika kwenye uwanja wa Magogo Mkoani Geita.
Mbio hizo za Mwenge ambazo zitahitimishwa Oktoba 14 mwaka huu
Mkoani Tanga zinaongozwa na kauli mbiu isemayo, “Elimu ni ufunguo wa maisha,
wekeza sasa kwa maendeleo ya nchi yetu”.
Vilevile Majaliwa alisema kuwa Mkoa wa Tabora unaongoza kwa
asilimia 9.7 ya wanafunzi watoro wa Sekondari ukifuatiwa na Geita (asilimia
8.1), Mtwara (asilimia 6.1) na Shinyanga (asilimia 6.3).
Kwa shule za Msingi, Rukwa inaongoza kwa asilimia 3.2,
ukifuata Geita (asilimia 3.1), Tabora (asilimia 2.9), Singida (asilimia 2) na
Simiyu (asilimia 2).
Alisema kwa jumla utoro wa wanafunzi wa sekondari ni mkubwa
kuliko shule za msingi huku akikumbusha kuwa Mikoa yote iliyotajwa juu ya
mapungufu hayo, kuhamasisha wananchi wake wakiwamo wazazi na walezi kuhusu
umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu ya watoto shuleni kwa kutumia utaratibu
wa sheria zilizowekwa.
No comments:
Post a Comment