Na Mwandishi wetu,
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Itikadi
na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey PolePole, amefunguka na kuwavaa
viongozi ambao wanazungumza juu ya ripoti ya CAG na kusema baadhi ya viongozi
hao wanapotosha umma kwa kusema mambo ya uongo.
Humphrey Polepole. |
Polepole alisema hayo leo wakati akizungumza
na Waandishi wa habari na kusema kuwa wapo viongozi wa vyama vya siasa
hawazungumzi juu ya mambo mazuri, yaliyofanywa na Serikali kama vile ujenzi wa
miundombinu na mambo wanayopiga hatua ila wamekuwa wakidakia mambo na kutoa taarifa
zisizokuwa na ukweli.
“Sasa unaposoma taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) halafu unatoa kauli timilifu kuwa
pesa imeibwa, yaani pesa ya umma imeibwa,
“Tunaweza tukakwambia tusaidie
kuthibitisha sasa ukishindwa umesema uongo umeuhadaa umma, umetoa takwimu za
uongo ukichukuliwa hatua sio ndiyo utaanza kusema uongozi huu hatuna huruma,
huruma kwa watu waovu? waongo wanaopotosha kwa makusudi hilo halikubaliki”,
alisema Polepole.
Aliendelea kueleza kuwa, “Mimi
sielewi huyu anayekwenda mbele kusema taarifa za uongo uongo hivi, ndiyo mtaji
wake siku hizi anatafuta tu pahala hoja hana, hazungumzi kuhusu rushwa siku
hizi hazungumzi kuhusu huduma za kijamii, hazungumzi kuhusu ufisadi, hazungumzi
kuhusu miundombinu, tunapiga hatua kubwa, tunapeleka watoto shule bure, bali
yeye anatafuta hoja ya uongo uongo”, alisema.
Polepole katika mkutano huo aliendelea
kumtuhumu mtu huyo kushindwa kuwa na uhakiki wa maneno yake.
“Kuna kipindi mtu huyu alizungumza
kuhusu njaa, wewe unaijua njaa inatangazwa vipi sasa tumevumilia sana leo
tumeshindwa tumeona tumsaidie kumuelewesha halafu tuseme wale ambao wana
dhamana ya kuhakiki maneno tunayatoa, kwa kweli wachukue hatua kwani hatupo
tayari kuacha watu wachache waendelee kuudanganya umma wa Watanzania hili halikubaliki”,
alisisitiza.
Pamoja na mambo mengine, mwishoni mwa
wiki iliyopita Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Zitto Kabwe
alizungumzia kwa mapana zaidi taarifa ya CAG na kuonyesha mambo ambayo Serikali
imetuhumiwa kufanya ikiwa pamoja na upotevu wa fedha zaidi ya trilioni 1.5
ambayo haina maelezo imetumikaje.
No comments:
Post a Comment