Baadhi ya Wanachama wa Mbinga Teachers SACCOS, Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma wakiwa jana kwenye Mkutano wao wa uchaguzi, ambao haukufanyika kutokana na idadi kamili ya wanachama wenzao kutotimia. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUTANO Mkuu wa uchaguzi wa kuwachagua
Viongozi wapya wa Chama cha Akiba na Mikopo, Mbinga Teachers SACCOS Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma jana Machi 31 mwaka huu, umeshindwa kufanyika kutokana na idadi
kamili ya Wanachama wa Chama hicho kushindwa kuhudhuria katika mkutano huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
ndani ya ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa ambako Mkutano huo
ulitarajiwa kufanyika hapo, baadhi ya Wanachama wa chama hicho walisema kuwa
tatizo hilo limesababishwa na wanachama wenzao kukata tamaa ya kuendelea kuwa
wanachama ndani ya ushirika huo kutokana na ubadhirifu wa mamilioni ya fedha,
uliofanywa na viongozi husika waliopewa dhamana ya kuendesha umoja wao.
Walisema kuwa licha ya kutoa kilio
chao kwa muda mrefu wakitaka vyombo vya dola na Serikali kwa ujumla, iingilie
kati kupitia Mrajisi wa Vyama vya ushirika Mkoani Ruvuma ili kuweza kunusuru
mali na fedha zao, hali hiyo bado imekuwa mbaya na ndiyo maana wamekata tamaa.
Adolph Komba ambaye ni mwanachama wa
chama hicho na pia Mwalimu wa shule ya msingi Luwino iliyopo kata ya Mkumbi
Wilayani hapa, alifafanua kuwa Maafisa ushirika wamekuwa ndiyo chanzo cha ubadhirifu
wa fedha zao ambapo wamekuwa wakiendekeza vitendo vya rushwa na kusimamia
utoaji wa mikopo isiyofuata taratibu na miongozo ya ushirika.
“Hata mimi binafsi nimekuwa
nikishangazwa na jambo moja, nimekuwa nikikatwa fedha katika mshahara wangu wakati
sina mkopo na sikukopa popote, lakini kila nikifuatilia namna ya kusitisha
mkopo ule na kurejeshewa fedha zangu zilizokatwa kimakosa hakuna shirikiano na utekelezaji
ninaoupata, nimekuwa nikizungushwa kila siku kwa kweli hali ya chama chetu ni
mbaya kuliko kama mnavyofikiria”, alisema Komba.
Komba aliongeza kuwa kutokana na hali
hiyo husababisha maendeleo ya chama hicho na yawanachama kwa ujumla wao kurudi
nyuma, hivyo kuna kila sababu sasa viongozi wa ngazi ya juu Serikalini kuingilia
kati kupitia Mrajisi wao wa Mkoa huo, kuingilia kati na kuchukua hatua kali za
kisheria juu ya kumaliza matatizo hayo yaliyopo.
Vilevile imeelezwa kuwa watumishi
ambao waliajiriwa katika chama hicho, wanalalamikiwa wakidaiwa kutofuata
taratibu husika za utoaji wa mikopo na kutoandaa taarifa za hesabu kikamilifu
kwa muda unaotakiwa.
Naye Charles Makenziye ambaye ni
mwanachama wa ushirika huo alieleza kuwa pia kumekuwa na madeni makubwa ndani
ya chama chao, kufuatia taasisi ya kifedha benki ya CRDB kuikopesha SACCOS hiyo
na kwamba mzigo wa madeni hayo umesababishwa na utendaji mbovu wa watendaji
waliokuwa madarakani katika chama hicho kwa kutozingatia taratibu husika.
Pia aliinyoshea kidole iliyokuwa bodi
ya mikopo ikilalamikiwa kwamba imekuwa haikuzingatia ushauri unaotolewa na
idara ya ushirika Wilayani Mbinga na ndiyo maana chama hicho kinaenda mrama.
Vilevile mikopo ambayo chama ilikopa
toka taasisi hiyo ya fedha imefikia hatua kutoingia kwenye mzunguko husika na
hali hiyo imesababisha sasa kutumia mtaji wa ndani kulipia madeni ya nje na
kukifanya kishindwe kusonga mbele kimaendeleo.
Naye Mjumbe wa bodi ya Mbinga
Teachers SACCOS, Aderick Kapinga aliwasihi wanachama wenzake akiwataka kuwa
watulivu na kupanga siku nyingine ya kuweza kufanya Mkutano huo na kuweza
kufikia suluhisho la matatizo hayo, ikiwemo kuwachagua viongozi wengine wapya
watakaoweza kuongoza chama hicho.
Pamoja na mambo mengine naye Afisa
ushirika anayesimamia vyama hivyo vya akiba na mikopo hapa Mbinga, Erasto
Msanga alisisitiza kwa kuwataka wapange tarehe nyingine ambapo walifikia
maamuzi kwamba Mkutano huo waufanye Aprili 28 mwaka huu na kwamba, matangazo yawafakie
wanachama wote kwa wakati ili waweze kuhudhuria siku hiyo kwa wingi na kuweza
kufanikiwa taratibu husika za kuweza kuwachagua viongozi hao wapya.
No comments:
Post a Comment