Na Kassian Nyandindi,
Songea.
IMEELEZWA kuwa changamoto ya ukosefu
wa vitendea kazi na uhaba wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya
ya Songea Mkoani Ruvuma, imechangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwenye
matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na
walimu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu Wilayani humo, kufuatia ziara
iliyofanywa na uongozi wa idara ya elimu katika kata 16 za Halmashauri hiyo kwa
lengo la kufanya tathimini ya kubaini changamoto zinazoikumba sekta hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
katika ziara hiyo, wadau hao walizitaja changamoto nyingine kuwa ni mwamko
hafifu wa wazazi katika kufuatilia maendeleo ya elimu kwa watoto wao, wazazi
kuhamia mashambani na watoto wao, uhaba wa walimu, uzembe wa walimu kuhudhuria
vipindi kwa wakati darasani, kufukuzwa kwa watoto mashuleni, vifo na magonjwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea
ilisajili jumla ya wanafunzi 3,389 kati ya hao wavulana walikuwa 1,678 wasichana
1,711 kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza mwaka 2011, ambapo waliosajiliwa
kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2017 walikuwa wanafunzi 2,706 kati yao
wavulana ni 1,281 na wasichana 1,418 na kwamba waliofanikiwa kufanya mtihani wa
kuhitimu darasa la saba katika mwaka huo ni 2,694 kati yao wavulana 1,281 na
wasichana ni 1,413 na kufanya jumla ya watahiniwa kuwa ni 2,694 sawa na
asilimia 99.55.
Kufuatia changamoto uwepo wa
changamoto hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Simon
Bulenganija kwa kushirikiana na wataalamu wengine wa elimu wameahidi kufuatilia
matatizo hayo na kuyatolea ufumbuzi wa haraka ikiwemo kufanya ukaguzi na
ufuatiliaji wa mara kwa mara mashuleni na kupeana maelekezo husika ili kuweza
kuondoa kasoro zilizopo.
Bulenganija alisema kuwa changamoto hizo
zilizojitokeza na kusababisha kushuka kwa ufaulu zitasaidia kupandisha ufaulu
kwa zaidi ya asilimia 85 kwa kipindi hiki cha mwaka 2018, ambapo Halmashauri
hiyo mwaka jana ilifaulisha kwa asilimia 67.7 na kushika nafasi ya tano kati ya
Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea
inajumla ya shule za msingi 71 kati ya hizo, mbili ni za taasisi ya dini ambazo
ni Chipole na shule ya mtakatifu Agnes Chipole.
No comments:
Post a Comment