Friday, April 20, 2018

MAKALA: KALINGA MILLERS MFANO WA KUIGWA MKOANI RUVUMA

Baadhi ya Wafanyakazi wa kiwanda kidogo cha Kalinga Millers, ambacho husindika unga wa Mahindi kilichopo Songea mjini Mkoani Ruvuma.
Unga wa Mahindi uliosindikwa na Kalinga Millers.

Na Dustan Ndunguru,

SERIKALI ya awamu ya tano imedhamiria Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025, juhudi zinazoendelea hivi sasa ni kuhamasisha uanzishaji wa viwanda hivyo kuanzia vidogo hadi vikubwa, hali ambayo itasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza ajira katika jamii.

Katika kuhakikisha mchakato huo unakuwa wenye ufanisi kunahitajika mipango mahusus ya kujenga viwanda vidogo, ukizingatia kwamba hasa katika sekta ya kilimo ndiko ambako malighafi huzalishwa kwa wingi.

Tunatambua ili viwanda hivyo viweze kuanzishwa kwa wingi hususan katika maeneo ya vijijini, miundombinu nishati ya umeme inatakiwa ijengwe huko kwa wingi na kwamba wataalamu wa sekta ya kilimo nao wanapaswa kuongeza juhudi katika kuelimisha na kujenga hamasa kwa wakulima waweze kuzalisha mazao ya aina mbalimbali, yenye ubora na hivyo mwisho wa siku kuweza kufanya viwanda vyetu vidogo na vile vikubwa tutakavyoanzisha kuwa endelevu na kuleta manufaa makubwa katika kukuza uchumi wetu.


Viwanda hivyo vidogo na vya kati ambavyo vitakuwa na uwezo wa kuajiri watu wengi vinapaswa kupewa kipaumbele kutokana na ukweli kwamba, vinahitaji gharama ya fedha kidogo ya uendeshaji tofauti na ikilinganishwa na viwanda vikubwa ambapo njia rahisi ni kuendelea kuhamasisha wakulima wajiunge kwenye vikundi vya uzalishaji mali ili kuweza kuwa rahisi kukopesheka na taasisi za kifedha kama vile benki.

Pia Serikali inaowajibu sasa wa kuangalia wafanyabiashara wadogo na wa kati wakiwemo wakulima wadogo juu ya namna ya kuwajengea uwezo wa kuwa na viwanda hivyo na kuachana na vitendo vya kuuza mazao wanayozalisha nje ya nchi jambo ambalo limekuwa haliwaletei tija na kuwafanya waendelee kubaki kuwa maskini.

Kama inavyofahamika kwamba miaka mingi iliyopita shughuli nyingi za uchumi zipo katika sekta ya kilimo hivyo iwapo Serikali itakuwa na dhamaira ya dhati ya kuboresha sekta hiyo ikiwemo miundombinu ya barabara za vijijini, umeme na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati na bei nafuu bila shaka wananchi wengi wataweza kufikia malengo husika.

Mkoa wa Ruvuma ni moja kati ya Mkoa ambao umeitikia mwito wa Serikali, kuhakikisha kwamba kasi ya uanzishaji wa viwanda inakuwa kubwa ili lengo la Serikali ya awamu ya tano liweze kufikiwa na kuweza kuwa na mafanikio.

Takwimu zinaonesha kuwa Mkoa huo mpaka sasa ina viwanda vidogo 185 na vikubwa saba idadi ambayo sote tunatambua kuwa ni ndogo ikilinganishwa na uwepo wa ardhi nzuri, inayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara hivyo jukumu lililopo mbele yetu ni kuhakikisha viwanda hivyo hususan vile vya usindikaji wa mazao vinaanzishwa ili kuweza kuyaongezea thamani mazao yetu.

Agizo la Serikali linawasihi Watanzania wajikite zaidi katika uanzishwaji wa viwanda hivyo na sasa limepokelewa vyema na wajasiriamali wengi hapa nchini, akiwemo mjasiriamali Ajira Kalinga ambaye anaishi katika Manispaa ya Songea Mkoani hapa.

Kalinga kwa ujumla ni mkulima ambaye hujishughulisha na shughuli za kilimo lakini ameamua kuanzisha kiwanda kidogo ambacho kinasindika unga wa mahindi mjini hapa na kufanya thamani ya zao la mahindi analozalisha liongezeke.

Kalinga anasema kuwa ni miaka mingi amekuwa akijihusisha na kilimo cha zao hilo na mpunga ambapo awali alikuwa akiuza bila kusindikwa lakini baada ya kuhudhuria semina mbalimbali za usindikaji mazao ameamua kuanzisha kiwanda hicho kidogo kilichopo mtaa wa Manzese hapa Songea kinachomwezesha kufanya usindikaji huo.

Anafafanua kuwa analo shamba la mahindi lenye ukubwa wa ekari 100 ambalo amekuwa akilima kwa kutumia trekta na kwamba wapo vijana watano, wamepata ajira ya muda kutokana na ujuzi wa kuendesha trekta hilo katika shughuli za kilimo.

“Changamoto nyingine kubwa ambayo nakabiliana nayo katika shughuli zangu za kilimo ni kutokuwepo kwa maduka ya pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na madawa ya kutokomeza wadudu waharibifu wa mazao jambo ambalo husababisha wakati mwingine niweze kukosa mazao mengi hasa wakati wa mavuno”, anasema Kalinga.

Anaiomba Serikali kupitia Wizara ya kilimo ifanye ufuatiliaji wa karibu na kuweza kubaini na kudhibiti wale wote ambao wamekuwa wakiuza dawa zisizokuwa na ubora, ambazo zimekuwa zikiumiza wakulima kwa kuwasababishia kuharibu mazao yao shambani na hatimaye kutofikia malengo ya kupiga hatua kimaendeleo katika sekta ya kilimo kama vile walivyotarajia.

Kalinga anasema Serikali inaowajibu wa kutupia jicho wajasiriamali wadogo kwa kuwapatia pia mikopo yenye masharti nafuu ambayo itawafanya wapate uwezo wa kuanzisha viwanda vidogovidogo ambavyo vitasaidia katika kukuza uchumi wao na nchi kwa ujumla sambamba na kuongeza ajira kwa vijana.

Anasema baada ya kufanikiwa kuanzisha kiwanda chake ambacho sasa anasindika unga wa mahindi na kukoboa mpunga maarufu kwa jina la “Kalinga Millers” amekuwa akipata mafanikio makubwa ambapo watu wengi wamekuwa wakijitokeza kununua unga anaosindika na mwingine hupeleka Mkoani Mtwara kwa ajili ya mauzo.

Anabainisha kuwa ili kukabiliana na changamoto ya ushindani wa biashara amekuwa akitengeneza bidhaa yenye ubora unaotakiwa na kukubalika katika soko la biashara.

Vilevile anapongeza jitihada za Rais Dokta John Pombe Magufuli katika ufufuaji na uanzishwaji wa viwanda hivi vidogo ikiwemo vya kusindika mazao, kwani kama hali hiyo itaendelea kuungwa mkono na Watanzania wengi juhudi hizi zitapata mafanikio makubwa na hivyo wengi wao kuweza kuondokana na umaskini uliokithiri miongoni mwao.

Kiwanda cha Kalinga Millers kimeweza hivi sasa kuajiri vijana 13 ambao wamekuwa wakifanya kazi kila siku na kwamba kadri kazi zitakavyokuwa zikiongezeka vijana wengine wataajiriwa ili nao waweze kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira.

“Lakini kikubwa nitoe wito kwa vijana wapende kujiunga na Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) ambavyo Serikali imejenga katika kila Mkoa na Wilaya, kwani kupitia huko watapata ujuzi zaidi ambao utawawezesha kupata ajira za muda au za kudumu katika viwanda vinavyotarajiwa kuanzishwa katika maeneo mengi hapa nchini, anasema.

Anasema kazi ya uanzishwaji wa viwanda hivi hapa nchini inapaswa kwenda na kazi ya kuhamasisha vijana walio wengi wajiunge na vyuo hivyo kwani changamoto mojawapo inayokuja mbele yetu, huenda viwanda vitakapokuwa tayari kuweza kuajiri vijana itakumbana na tatizo la kukosekana kwa wale wasiokuwa na sifa ya kuajiriwa kutokana na kukosa elimu husika hivyo mwisho wa siku watakosa ajira.

Naye Omary Kadewele mmoja kati ya mwajiriwa katika kiwanda hicho cha kusindika unga anasema kuwa kabla ya kufanikiwa kupata kazi kiwandani hapo, alikuwa akipoteza muda mwingi vijiweni ambapo maisha yake yalikuwa magumu lakini sasa anao unafuu mkubwa katika maisha kwani hana tatizo lolote kutokana na ukweli kwamba anamudu majukumu ya kuendesha maisha yake ikiwemo kununua chakula na mavazi.

Alli Kwambiana vilevile anaeleza kuwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho kumemfanya apate ajira ya muda inayomwezesha kupata riziki yake ya kila siku ikilinganishwa na hapo awali, ambapo alikuwa akizurura mitaani bila kazi ya kufanya huku akishindwa kumudu gharama mbalimbali ikiwemo kulipa pango kwenye nyumba anayoishi.

Msimamizi Mkuu wa kiwanda hicho cha kusindika unga wa mahindi, Iddi Kalinga anabainisha kuwa dhamira yake ni kuendelea kuzalisha bidhaa yenye ubora ili wateja wake waweze kuendelea kununua huku akiongeza kuwa pale ambapo wanahisi kuna tatizo wateja wasisite kutoa taarifa ili hatua husika ziweze kuchukuliwa.

Anapongeza Serikali kutokana na uamuzi wake wa kupeleka umeme katika maeneo ya vijijini kwani wanafikiria pia kuwekeza kwenye maeneo hayo ya vijijini.

Pamoja na mambo mengine, siku zote sekta ya kilimo itaendelea kubaki kuwa ndiyo msingi mkuu wa kukuza uchumi Tanzania kutokana na ukweli kwamba hutoa asilimia 95 ya mahitaji ya chakula na kutengeneza ajira kwa asilimia 66 ya idadi ya watu na malighafi ya viwanda.

Jukumu lililopo sasa ni kwa Serikali kuendelea kuwaunga mkono wazalendo ambao wameitikia mwito wake wa kuanzisha viwanda vidogo au vikubwa, ili viweze kusonga mbele badala ya kurudi nyuma kama ilivyokuwa kwa viwanda ambavyo vilikuwepo miaka ya nyuma na baadaye kupotea.

Kinachotakiwa pia ni kwa wale ambao wanabahatika kupata ajira katika viwanda hivyo, kujenga tabia ya uaminifu pindi wanapokuwa kazini kwani kufanya hivyo vitaweza kusonga mbele na lengo la Serikali la kukuza uchumi wake wa viwanda kuweza kufikiwa na kutekelezwa ipasavyo kwa vitendo huku Viongozi wa kuchaguliwa na Watendaji wa Serikali Mkoani Ruvuma, wanaowajibu wa kuhakikisha kwamba wanahamasisha wananchi wajikite zaidi katika kuanzisha viwanda hivyo ili viweze kuwa endelevu.
 

No comments: