Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WATOTO yatima na wale wanaoishi
katika mazingira hatarishi Wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma, wametakiwa
kujiepusha na vitendo viovu vya matumizi ya dawa za kulevya ili wasiweze
kuharibu afya zao.
Aidha watoto hao wameaswa kujiepusha
na wanaume walaghai ambao wanaweza kuwapotezea ndoto za maisha yao ya baadaye,
badala yake wanapaswa kusoma kwa bidii na kuwa viongozi wazuri wa kuliongoza
taifa hili.
Mgema alisema hayo juzi alipokuwa kwenye
hafla fupi ya kuwaaga watoto hao katika kituo cha Mwangaza, ambao wamefikia
ukomo wa kuishi kituoni hapo huku akitoa pongezi kwa uongozi wa kituo kwa kuwasomesha
hadi kufikia ngazi ya vyuo vikuu.
Alisema kuwa kitendo hicho kilichofanywa
ni cha mfano wa kuigwa kwani kumekuwa na baadhi ya watu wakianzisha asasi, kwa
lengo la kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi lakini
mara baada ya kupata ufadhili huwageuza watoto hao kama kitega uchumi cha
kunufaisha matumbo yao.
Pia Vermunda Njawike awali akizungumza
kwa niaba ya watoto wenzake alisema kuwa wanaushukuru uongozi wa kituo kwa
kuwapatia huduma ya chakula, mavazi, malazi, afya na elimu huku akiwataka
watoto wenzake kuendelea kuishi katika maadili mema na kuzingatia masomo
darasani.
Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi
wa kituo hicho, Anna Mugenya ameitaka jamii kuacha tabia ya ubinafsi na badala
yake wajenge utamaduni wa kujitoa katika kusaidia watoto yatima na wanaoishi
katika mazingira hatarishi, huku akieleza kuwa jukumu la kuwalea watoto hao ni
kila mtu.
Aliyataja mafanikio mbalimbali yaliyotokana
na kuwasomesha watoto hao ni pamoja na baadhi yao kujiunga na Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) na wengine kuajiriwa pamoja na kujiendeleza katika fani
mbalimbali.
Kituo cha Mwangaza
kimekuwa kikipata ufadhili wa kulea watoto hao kutoka nchi ya Japan na Marekani
na kwamba wameweza kupata mafanikio mengine, kwa kuendelea kujenga makazi ya
kudumu ya kituo hicho katika eneo la Mwengemshindo hapa mjini Songea ikiwemo
pia jengo la kulelea watoto wachanga.
No comments:
Post a Comment