Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
IDADI ya Wananchi wanaopata huduma ya
maji safi na salama katika Mji wa Tunduru Mkoani Ruvuma, imeongezeka kutoka 23,200
mwaka 2016/2017 hadi kufikia wananchi 32,200 katika kipindi cha mwaka huu.
Aidha kutokana na maboresho ya
mitambo na vyanzo vya maji yanayoendelea kufanywa na Mamlaka ya Maji safi
na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Tunduru (TUWASA) hivi sasa mgawo wa maji
umepungua kwa baadhi ya maeneo ikiwemo Jeshi la magereza, Hospitali ya Wilaya,
kambi ya Polisi na maeneo mengine katika mji huo.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Mamlaka
hiyo, Christopher Mbunda wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini
hapa, ambapo alisema TUWASA imeweza kuwa na wateja 1,590 na kati ya hao
waliofungiwa mita ni 1,460 na wasio na mita ni 130.
Alisema kuwa wanatarajia kumaliza
kuwafungia mita wateja wote waliobakia ifikapo Desemba mwaka huu, hatua ambayo
itasaidia kuongeza mapato ya Mamlaka hiyo.
Kwa ujumla mahitaji ya maji kwa kwa
siku kwa wakazi wa Mji wa Tunduru ni lita milioni 2,919,420 lakini wananchi
wanaopata huduma ya maji safi na salama ni 32,200 sawa na asilimia 66 na kwamba
wananchi waliounganishwa kwenye bomba kuu la kusambaza maji hayo ni 1,514.
Mbunda alieleza kuwa uzalishaji wa
maji kwa siku umeongezeka kutoka lita 1,500,000 hadi kufikia lita 1,968,000 hivyo
hali ya uzalishaji wa maji kwa sasa hufikia asilimia 67 kutoka asilimia 54 ya
mwaka 2016/2017.
Miundombinu ya maji iliyopo
Tunduru mjini ilijengwa tangu mwaka 1,953 hivi sasa imechakaa jambo ambalo
linasababisha mtandao wa bomba la kusambazia maji kutofika maeneo mapya ya mji,
hivyo baadhi ya maeneo kukosa huduma na kulazimika kutumia maji ya kisima.
Aliongeza kuwa licha ya mafaniko hayo
bado kuna changamoto kubwa zinazoikabili Mamlaka hiyo ikiwemo uchakavu wa
miundombinu ya maji, gharama kubwa ya umeme kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya
kuzalisha maji, pamoja na baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa ankara za maji
kwa wakati.
Katika kukabiliana na changamoto hizo
Mbunda alisema wameomba fedha kutoka Wizara ya maji Shilingi milioni 300 kwa
ajili ya kukarabati na kuongeza mtandao wa maji huku akiliomba Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) kusaidia kurekebisha mfumo wa umeme hasa kwenye mitambo ya kusukumia
maji.
No comments:
Post a Comment