Mandhari ya bustani ya Manispaa Songea Mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MRADI wa bustani ya Manispaa ya Songea
uliopo Mkoani Ruvuma, umekamilika na kwamba unatarajia kuanza kufanya kazi mwishoni
mwa mwezi Mei mwaka huu, ambapo Mkandarasi husika tayari amekabidhi mradi huo kwa
uongozi wa Manispaa hiyo.
Kaimu Mkuu wa idara ya ujenzi wa Manispaa
hiyo, Mhandisi Nicolous Danda alisema kuwa mradi huo ulikamilika tangu mwezi Desemba
mwaka 2017 huku Mkandarasi aliyepewa jukumu la ujenzi wa bustani hiyo akipewa matazamio
ya miezi sita ya ujenzi wa mradi huo ambayo inaishia mwezi Aprili mwaka huu.
Danda amezitaja kazi zilizosalia katika
mradi huo kuwa ni kuendelea kuotesha nyasi, kufunga mfumo wa maji taka ambayo inafanywa
na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (SOUWASA) na kuweka nishati ya Umeme kazi ambazo
zinatarajia kukamilika mapema mwezi huu.
“Wakati wowote kuanzia sasa tunatarajia
kitengo cha manunuzi kutangaza zabuni, hivyo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei
mwaka huu tunatarajia bustani kuanza kazi’’, alisema Mhandisi Danda.
Kwa ujumla mradi huo umefadhiliwa na Benki
ya dunia kwa gharama ya Shilingi milioni 399 na kwamba mradi huo hadi kukamilika
kwake umetumia Shilingi milioni 444, fedha zote ikiwa ni za mradi wa Benki hiyo.
Wawakilishi wa Benki ya dunia wameukagua
mradi huo na kuridhishwa na kiwango cha ujenzi uliofanyika wa bustani hiyo ambayo
inavutia wengi kwa kuwa imebadilisha muonekano wa Mji wa Songea.
Mradi huo unaofadhiliwa na Benki hiyo
chini ya Mpango wa Kuzijengea Uwezo Serikali za Mitaa (ULGSP) una eneo la
mgahawa, choo cha kulipia, uzio, maeneo ya kupaki magari (Parking bay), eneo la
kupumzikia (Resting huts), maeneo ya kuchezea watoto na inatarajia kuwa na Kituo
cha kutolea habari za utalii na uwekezaji za Manispaa na Mkoa wa Ruvuma.
No comments:
Post a Comment