Na Dustan Ndunguru,
Tunduru.
VIONGOZI wa vyama vya ushirika Wilayani
Tunduru, Mkoa wa Ruvuma wametakiwa kusimamia kikamilifu hesabu za vyama hivyo,
ili viweze kuwanufaisha wanachama wake na kuvifanya kuwa endelevu.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Homera
alisema kuwa viongozi wengi wa vyama ushirika hapa nchini wamekuwa legelege
katika kufuatilia mikopo wanayotoa kwa wanachama wao, na kushindwa kusimamia hesabu
ipasavyo za uendeshaji wa ushirika huo na mwisho wa siku husababisha kuyumba
na kufa kabisa kwa vyama vya ushirika.
Alisema kuwa wanachama wa vyama hivyo
wanatakiwa kujenga mazoea ya kulipa mikopo waliyokopeshwa kwa wakati, ili kuweza
kutoa nafasi kwa wanachama wengine waweze kukopa.
Homera alisisitiza kuwa imekuwa ni
mazoea miongoni mwa wanachama kuona fahari kwamba fedha wanazokopa kuwa ni mali
yao, kwa kutoirejesha kwenye vyama hivyo jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo
husika.
Alisema kuwa ni aibu kwa mwanachama
kufukuzwa ndani ya ushirika baada ya kushindwa kurejesha mkopo aliokopa kwa
hiari yake bila kulazimishwa, jambo ambalo halipendezi kwa sababu linaondoa
imani na uaminifu wake hususan katika vyombo fedha kama vile benki.
Mkuu huyo wa Wilaya Tunduru aliwataka
pia wanachama hao kutumia vyema mikopo wanayokopeshwa na kwamba waepuke vitendo
vya anasa ambavyo huwafanya washindwe kuondokana na umaskini unaowakabili
miongoni mwao.
Alisema dhamira kubwa ya Serikali ya
awamu ya tano ni kuona vyama vyote vya ushirika vinafanya kazi kwa umakini
mkubwa ili wananchi waweze kunufaika navyo huku akongeza kuwa haitasita
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaonekana kutaka kuzorotesha
maendeleo ya ushirika.
No comments:
Post a Comment