Friday, April 6, 2018

WANUFAIKA TASAF TUNDURU WAANZISHA SHAMBA LA MITI YA MBAO


Na Kassian Nyandindi,         
Tunduru.

WALENGWA waliopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini kijiji cha Mchesi kata ya Mchesi, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma kupitia ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wameanzisha shamba la miti ya mbao, aina ya Mitiki lenye ukubwa wa ekari nne.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho ambaye pia ni mlezi wa wanufaika hao waliopo katika mpango huo, Lazima Mrope alisema kuwa katika ekari hizo tayari wamepanda jumla ya miti 1,200 ya mbao kati ya miti 4,000 iliyopo kwenye mpango wa kuipanda ikiwemo miti ya matunda na kwamba miti iliyobaki imegawiwa bure kwa wanufaika ambao wamepanda katika mashamba yao binafsi.

Mrope alifafanua kuwa mbali na miti hiyo ya mbao pia wameanzisha kilimo cha mahindi, ambayo mara yatakapokomaa wanufaika watakuwa na uhakika wa kuweza kupata chakula katika msimu wote wa mwaka, badala ya kusubiri ruzuku inayotolewa na Serikali ambayo hata hivyo haitoshelezi mahitaji yao.


Alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuboresha maisha ya kaya maskini ambazo zinapokea fedha za ruzuku kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF 111 chini ya mpango huo wa kunusuru kaya maskini.

Alibainisha kuwa tangu Serikali ilipoanzisha utaratibu wa kutoa ruzuku kwa baadhi ya kaya, mfumo huo umesaidia baadhi ya kaya kutoka katika matatizo ya umaskini kwa kuanzisha vikundi vidogo vidogo vya kukuza uchumi wao na ujenzi wa nyumba bora za kuishi.

Vilevile kupitia miradi iliyofanywa na wanufaika hao kwa kushirikiana na jamii iliyopo kijijini, imeweza kusaidia hata upatikanaji wa huduma muhimu kama vile afya na maji ambapo hata jamii hivi sasa imehamasika kushiriki katika kazi za kujitolea.

Mratibu wa TASAF Wilaya ya Tunduru, Muhidin Shaibu alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 Mfuko huo kwa kushirikiana na walengwa imepanda miti rafiki ya maji kwenye vyanzo vya maji, miti ya mbao na matunda katika mashamba.

Aliongeza kuwa mbali na kupanda miti pia katika mwaka huo wametekeleza na kukamilisha miradi 74, kudhibiti korongo 1, kutengeneza mbolea ya asili katika vijiji 52, kuboresha visima vya maji 35 na ujenzi wa mabwawa ya samaki 10.

Shaibu aliitaja miradi mingine kuwa ni ya umwagiliaji wa maji, barabara za mitaa, vivuko vya miguu, kuchimba lambo katika vijiji sita na mradi wa kuhifadhi maji ya mvua katika vijiji vya Wilaya hiyo.

No comments: