RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe
Magufuli leo Aprili Mosi mwaka huu ameungana na Wakristo wote katika
maadhimisho ya Misa Takatifu, ya sikukuu ya Pasaka iliyofanyika kwenye Kanisa
la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kukaribishwa na Padri Venance Tegete
kutoa salamu, Dokta Magufuli amewatakia Watanzania wote heri ya sikukuu hiyo
huku akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuishi kwa amani, upendo na kushiriki
kikamilifu katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa hili.
“Kifo na ufufuko wa bwana wetu Yesu Kristo ukafufue matendo
yetu, tuendelee kuijenga amani yetu, upendo wetu na tujenge maendeleo ya Watanzania
wote, kwani Kristo alitufundisha upendo miongoni mwetu,
“Kwa hiyo Baba nakushukuru sana kwa kuongoza misa hii, naomba
ufikishe shukrani zangu kwa Kardinali Pengo, Maaskofu wote na Watanzania wote
tuendelee kusimama pamoja ili tulijenge Taifa letu”, alisema Dokta Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, Dokta Magufuli alikuwa ameongozana
na mkewe Mama Janeth Magufuli katika misa hiyo ambayo ilikuwa ikiongozwa na
Paroko wa Kanisa hilo, Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Padri Venance
Tegete.
No comments:
Post a Comment