Na Kassian Nyandindi,
Songea.
SERIKALI katika kipindi cha kuanzia
mwezi Julai mwaka jana hadi kufikia Machi mwaka huu, tayari imetumia jumla ya
Shilingi bilioni 4,894,932.063 Mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuboresha mazingira
ya elimu.
Christine Mndeme. |
Aidha huo ni mkakati wake wa
kuwezesha mpango wa elimu bila malipo kwa shule za Msingi na Sekondari Mkoani
humo uweze kuwa endelevu.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine
Mndeme alisema hayo alipokuwa akizungumza na Wadau mbalimbali wa elimu Mkoani
hapa katika kikao cha tathimini ya elimu kilichoketi kwenye ukumbi wa Manispaa
ya Songea mjini hapa.
Alisema kuwa ni jambo la kumshukuru
Rais Dkt. John Magufuli kwa jitihada zake za kuboresha mazingira ya elimu hapa nchini
ambapo ameweza pia kutoa vifaa vya maabara kwenye shule za Serikali, jambo
ambalo sasa linasaidia watoto shuleni waweze kusoma masomo ya Sayansi kwa
vitendo bila usumbufu wa aina yoyote ile.
Hatua hiyo Mndeme alieleza kuwa
imewezesha wanafunzi hao kufanya vyema katika masomo na mitihani yao hatimaye
kuweza kuondokana na aibu ya watoto kuendelea kufanya vibaya.
Katika matokeo ya mitihani ya miaka
mitatu iliyopita ufaulu katika Mkoa huo umekuwa ukishuka, kwani matokeo ya
darasa la saba kutoka yalikuwa asilimia 68.4 mwaka 2015 hadi asilimia 66.26
mwaka 2016 na asilimia 64.2 mwaka 2017.
Alisema kutokana na ufaulu huo Mkoa umeshuka
kutoka nafasi ya 11 mwaka 2015 na kushika nafasi ya 16 mwaka 2016, hadi kufikia
nafasi ya 21 katika ngazi ya kitaifa mwaka 2017, huku asilimia ya ufaulu kwa
mitihani ya darasa la saba mwaka 2016 ilikuwa asilimia 66.28 hivyo kupungua kwa
asilimia 2.08 mwaka 2017.
Kwa upande wa mitihani ya kidato cha
nne Mndeme alisema ufaulu umekuwa sio imara toka asilimia 74.58 ya mwaka 2015,
asilimia 82.29 mwaka 2016 hadi asilimia 77.28 ya mwaka 2017 huku mwaka 2015 Mkoa
ukishika nafasi ya 7, nafasi ya nane mwaka 2016 na nafasi ya 25 kati ya mikoa
30 mwaka 2017.
Mndeme aliongeza kuwa changamoto kubwa
iliyosababisha kuwa na matokeo mabaya ni utoro, ufundishaji usiokidhi viwango,
viongozi katika ngazi mbalimbali kutofanya ufuatiliaji, upungufu wa baadhi ya
vifaa vya kujifunzia, kufundishia na mimba za utotoni kwa watoto wa kike.
Katika kukabiliana na tatizo la mimba
Mkuu huyo wa mkoa amepiga marufuku walimu na wakuu wa shule zote za Msingi na
Sekondari kuwapokea wanafunzi waliopata ujauzito, ambapo ameitaka jamii kuhakikisha
kwamba wanapambana kupiga vita mimba za utotoni ili kutoa fursa kwa wanafunzi
wa kike waweze kusoma na hatimaye kutimiza ndoto zao.
No comments:
Post a Comment