Na Albano Midelo,
Songea.
MANISPAA ya Songea Mkoani Ruvuma kwa
kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, wiki ya mwisho wa mwezi Machi mwaka
huu iliweka kituo cha wananchi kujitolea damu katika viwanja vya Soko kuu mjini
Songea.
Uchunguzi umebaini kuwa asilimia 80
ya wanaohitaji damu hapa nchini ni wanawake, kwa sababu mbalimbali ikiwemo
uzazi salama wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida na njia ya
upasuaji.
Katika kipindi cha siku tatu za uhamasishaji
wa wananchi kujitolea damu, lengo lilikuwa ni kukusanya uniti 100 za damu.
Vilevile kuanzia Machi 27 hadi 29 mwaka
huu kitengo cha damu salama katika kituo cha Soko hilo kilikuwa kimekusanya uniti
67.
Changamoto kubwa iliyosababisha
kutofikia malengo ya kukusanya uniti 100 kwa siku tatu ni kutokana na kufungwa
kwa shule za Sekondari, kwa ajili ya kwenda mapumziko ya sikukuu ya Pasaka hali
ambayo imesababisha watu wachache kujitolea damu salama.
Kadhalika imebainika kuwa watu
wanaoongoza kujitolea kutoa damu ni wanafunzi wa shule za Sekondari na taasisi zingine
kama vile Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Jambo la msingi ni kuendelea kutoa
elimu ya kujitolea damu kwa Watanzania kwa kutumia vyombo vya habari, matangazo,
mikutano ya hadhara hali ambayo itaweza kuhamasisha wananchi wengi kwa kiasi
kikubwa kuona umuhimu wa kujitolea damu ili vituo vya afya na hospitali ziweze
kuwa na benki ya kutosha ya damu salama.
Mpango wa Taifa wa damu salama
umesema kuwa Jamii Kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kujitolea
damu, imekuwa ni kikwazo kikubwa namba moja kwa mpango huo kushindwa kufikia
malengo ya ukusanyaji wa damu salama kutoka kwa wananchi.
Kuna wale wanaoamini kwamba kujitolea
damu ndiyo mwanzo wa kubomoa mfumo sahihi wa mzunguko wa damu na kuna
wanaoamini kuwa kujitolea damu ndiyo kujiletea ugonjwa wa shinikizo la damu.
Fikra hizo ndizo zinanidhihirishia wazi
kuwa katika umma huu wa Watanzania, wapo wasioelewa mambo mengi muhimu kuhusu
kujitolea damu, hivyo kusababisha utoaji damu kwa hiyari kuwa mgumu.
Kuna umuhimu sasa wahusika waliopewa
dhama kutekeleza jambo hilo kuweka utaratibu mzuri, wa kuhakikisha elimu sahihi
kuhusu umuhimu wa watu kujitolea damu inawafikia hata wananchi wanaoishi vijijini.
Maneno hayo yanayozungumzwa na
wasioelewa kuhusu umuhimu wa kutoa damu ni mengi, kwa hiyo wahusika waichukulie
hiyo kuwa ni changamoto kubwa inayopaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili
hatimaye, tatizo la upungufu wa damu katika vituo vyetu vya kutolea huduma za
afya libakie kuwa historia.
No comments:
Post a Comment