Na Muhidin Amri,
Songea.
BAADHI ya Wakazi kumi wanaoishi
katika maeneo mbalimbali Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, wamepigwa faini ya
shilingi Milioni moja kwa ujumla wao baada ya kubainika wamekataa kulipa
shilingi 2,000 ambayo inatozwa kila mwezi kwa kila kaya, kwa ajili ya kuchangia
huduma za usafi wa mazingira katika Manispaa hiyo.
Mahakama ya Mwanzo Mfaranyaki iliyopo
mjini hapa, ndiyo iliyowahukumu adhabu hiyo na kwamba Wakazi hao ni wale wa kutoka
katika kata ya Majengo, Misufini, Bombambili na Matarawe.
Philipo Beno ambaye ni Mkuu wa
masuala ya usafi wa mazingira katika Mnispaa ya Songea akizungumza juzi na Waandishi
wa habari, alisema kuwa wameamua kuanza kuwapeleka Mahakamani Wananchi wote
wanaonekana kukaidi kulipa mchango huo, ili iweze kuwa fundisho kwa wengine
wenye tabia kama hiyo na hatimaye waweze kuchangia kwa urahisi bila usumbufu
wowote kwa kufuata taratibu na sheria ndogo zilizowekwa.
“Sheria imepitishwa kwamba kila mwezi
wanatakiwa kuchangia shilingi 2,000 kwa kila kaya na kwa upande wa
Wafanyabiashara, hawa wanachangia shilingi 4,000 ili tuweze kufanya usafi wa
mazingira kwa ufasaha kwenye mitaa na kata zetu zilizopo katika Manispaa hii”,
alisema Beno.
Alifafanua kuwa baada ya kukataa
kuchangia mchango huo, waliona ni vyema wapelekwe katika Mahakama hiyo ambako
katika hao kumi kila mmoja alipigwa faini ya shilingi 100,000 huku akiongeza
kuwa, kuanzia sasa zoezi la kuwapeleka Mahakamani litakuwa endelevu kwa wale wote
watakaokuwa wakikaidi kutekeleza suala hilo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya
ya Songea Pololet Mgema naye amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Songea
Mkoani hapa, kupitia Maafisa wake wa afya kuendelea kuhamasisha wananchi
kushiriki kikamilifu zoezi la usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa
mwezi, ambayo ndiyo ni siku maalum ya kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya
umma.
Alitoa agizo hilo huku akieleza kuwa
wananchi wengi wa Songea wamekuwa hawashiriki kikamilifu katika siku hiyo ya
usafi hivyo kwa wale wanaokaidi wanapaswa kuchukuliwa hatua.
Mgema amewaagiza pia Watendaji wa
mitaa 95 iliyopo mjini hapa kuorodhesha majina ya wale wote wanaokataa
kushiriki kufanya usafi huo wa mazingira, ili waweze kupigwa faini ya shilingi
50,000 kila mmoja kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Alisisitiza kuwa usafi wa mazingira
ni jambo la lazima na sio hiari ili kuweza kukabiliana na magonjwa
yanayosababishwa na uchafu na kwamba, utafiti umebaini kuwa nchi zilizoendelea
hapa duniani zimekuwa zikishangaa kusikia au kuona watu wanaugua na kupoteza
maisha kutokana na magonjwa yatokanayo na uchafu.
No comments:
Post a Comment