Monday, March 19, 2018

WAHUDUMU WA AFYA MKAKO MBINGA WAZALISHA MAMA WAJAWAZITO KWA KUTUMIA MWANGA WA SIMU ZA MKONONI

Amina Makillagi.

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WAHUDUMU wa Afya wanaofanya kazi katika Zahanati ya Mkako iliyopo Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wamefikisha kilio chao kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Amina Makillagi wakilalamikia kwamba kutokana na kukosa mwanga wa umeme kwenye zahanati hiyo, nyakati za usiku wamekuwa wakizalisha akina mama wajawazito kwa kutumia mwanga wa simu za mkononi huku wakiwa wameziweka mdomoni.

Aidha walisema kuwa kwa kulinda hadhi ya mwanamke wanahitaji Serikali iboreshe mazingira ya zahanati hiyo, ikiwemo chumba cha kujifungulia akina mama hao ambacho hivi sasa hakina mazingira rafiki hasa pale wanapotoa huduma husika.

“Tumekuwa tukipata tatizo la mwanga tunapotoa huduma nyakati za usiku, tunazalisha akina mama 10 hadi 15 kwa mwezi kwa kutumia mwanga wa simu za mkononi tumeahidiwa kwa muda mrefu kuletewa umeme, lakini tunaomba tuharakishiwe ili tufanye kazi zetu kwa ufanisi zaidi”, walisema.


Grace Gaya ambaye ni Muuguzi msaidizi akiwa na baadhi ya Watumishi wenzake, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya zahanati ya Mkako mbele ya Katibu Mkuu wa UWT Taifa, Makillagi huku akifafanua kuwa kwa mwezi wamekuwa wakihudumia wagonjwa 420 wenye magonjwa mbalimbali.

Muuguzi huyo aliongeza kuwa changamoto nyingine inayowakabili kituoni hapo ni pamoja na upungufu wa kitanda cha kujifungulia akina mama hao, kwani kilichopo ni kimoja tu na hakitoshelezi mahitaji huku kukiwa na tatizo kubwa la upungufu wa watumishi kutokana na mlundikano wa wagonjwa.

Alisema kuwa changamoto hiyo ni pamoja na upungufu wa vifaa tiba ikiwemo dawa za kutibu watoto wadogo na kwamba, wagonjwa wengi wanaopatiwa matibabu hapo ni wale ambao wanatokana na magonjwa yanayoambukiza kwa njia ya hewa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa akina mama Tanzania, Makillagi alisema kuwa kituo hicho cha afya ni chakavu kinahitaji ukarabati ufanyike haraka ili kuweza kuendelea kuimarisha afya na huduma muhimu za wananchi.

“Poleni sana mnafanya kazi kwenye mazingira magumu, zahanati ni chakavu inaonekana haijakarabatiwa kwa muda mrefu UWT tumejipanga na Serikali, kushughulikia kero hizi”, alisisitiza.

Baada ya kutembelea zahanati hiyo, kupitia Umoja huo wa wanawake aliahidi kuwapatia vitanda viwili vya kujifungulia akina mama wajawazito pamoja na kushughulikia kero ya uhaba wa watumishi.

Hata hivyo zahanati imekuwa ikihudumia vijiji mbalimbali vilivyopo Wilayani Mbinga, ambavyo ni Kihuruku, Lihale, Kigombi, Amani makolo na Mkako.

No comments: