Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) Amina Makillagi amesema kwamba, Viwanja vyote ambavyo vina
migogoro na ni mali ya umoja huo Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wale wote
ambao wamekuwa wakivitaka wakidai kuwa ni vya kwao wavirudishe mapema kabla
hawajachukuliwa hatua kali za kisheria.
Alisisitiza kuwa yeyote aliyepora
mali za Umoja huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Dokta
John Pombe Magufuli atapelekewa ripoti ili waweze kushughulikiwa.
“Popote walipo hao ambao wamepora
viwanja vyetu warudishe mara moja hatutaki utani, niwasihi na kuwaomba waachane
na ubinafsi warudishe mali zetu”, alisisitiza Makillagi.
Agizo hilo alilitoa juzi alipokuwa
akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa huku akisisitiza kuwa palipokuwa
na mali ya UWT wanao ushahidi wa kutosha kwamba, ndiyo mali ya Umoja huo hivyo
anatambua kuwa Mahakama ndiyo chombo cha kisheria ambacho mwisho wa siku
kitasimamia haki yao.
Makillagi alisisitiza kuwa katika
wiki mbili kuanzia sasa anataka awe amepewa taarifa mezani kwake kwamba, viwanja
vyote vya Umoja wa wanawake hapa nchini, vimepimwa vikisubiri tayari kupewa
hati miliki ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.
Amewataka Wakurugenzi katika
Halmashauri husika kwa kushirikiana na viongozi wa UWT, wahakikishe wanatoa
ushirikiano wa kutosha katika upimaji wa viwanja hivyo ili hapo baadaye viweze
kuleta manufaa kwa jamii.
“Kufika wiki mbili nataka niwe
nimepata majibu juu ya hili agizo langu nililolitoa kwa viwanja vyote ambavyo
ni mali yetu akina mama wa umoja huu wa wanawake, tutaleta mwanasheria wa
kushughulikia matatizo haya na gharama zote za kushughulikia hili tutalipa
chama Jumuiya ya UWT”, alisema.
Pia Katibu huyo alitumia msemo akisema
kuwa “mali bila daftari hupotea bila habari”, hivyo kuna kila sababu ya
kudhibiti mali na mapato ya chama kupitia miradi mbalimbali, huku viongozi
ndani ya chama wakitengeneza ratiba ya kutembelea wanachama katika maeneo yao
wanayoishi kwani wanaCCM wanahitaji kusogelewa karibu.
Pamoja na mambo mengine alisisitiza
kuwa mali zote ndani ya Chama zimekuwa zikimilikiwa na Baraza la Wadhamini
Taifa, hivyo kazi ya baraza hilo ni kusimamia mali hizo na kuhakikisha kwamba
hakuna inayopotea.
No comments:
Post a Comment