Sunday, March 18, 2018

DED MADABA AMTUMBUA AFISA MANUNUZI


Na Muhidin Amri,         
Madaba.

UKIUKAJI wa taratibu za manunuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, ambako kumefanywa na Mkuu wa idara ya Manunuzi katika Halmashauri hiyo, Boniface Soko kumemfanya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Shafi Mpenda kumsimamisha kazi mtumishi huyo.

Mpenda alisema kuwa, Soko amekuwa akifanya hivyo kwa makusudi na kwamba Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imekuwa ikisisitiza na kutoa miongozo mara kwa mara namna ya kutumia mfumo wa Force Account, lakini yeye hazingatii hilo.

Alisema kuwa mfumo huo umekuwa mzuri kwani unalenga kutumia mafundi wanaopatikana katika jamii, badala ya kutumia Makandarasi ili kuweza kuepuka gharama kubwa ambazo Serikali imekuwa ikitumia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.


“Kimsingi akiwa ni mtaalamu ambaye nilikuwa nikimuamini na kumteua Katibu wa kamati ya manunuzi ndani ya Wilaya, kama mwongozo unavyoelekeza kwamba maafisa ugavi kuwa sehemu ya muundo wa kamati hiyo”, alisema Mpenda.

Vilevile alibainisha kuwa cha kushangaza aliamua kutumia mfumo wa kikandarasi kutengeneza nyaraka husika akiaminisha kuwa ndiyo mfumo sahihi wa Force Acount, hali ambayo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa uongozi wa Wilaya katika kutekeleza miradi miwili ya Vituo vya afya vilivyopo Wilayani humo.

Mpenda alifafanua kuwa, Soko alitengeneza malipo ya shilingi Milioni 8 na kuyapeleka Ofisi ya Mkurugenzi huyo ili aweze kumpitishia (Posho) kwa ajili ya kufanya malipo mbalimbali bila kupitisha kwenye kamati husika ya manunuzi ili iweze kuridhia juu ya malipo hayo.

Hivi sasa jambo hilo lipo katika hatua ya uchunguzi wa awali kwa kutumia kanuni ya 36 ya kanuni za kudumu, katika utumishi wa umma za mwaka 2003 ili kuweza kubaini chanzo cha madai hayo.

“Sipo tayari kuona utaratibu wa kisheria ikiwemo na maelekezo ya Serikali kutozingatiwa katika Halmashauri hii, mtumishi atakayefanya hivyo sitosita kumshugulikia”, alisisitiza.

No comments: