Na Mwandishi wetu,
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli
amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
kuhakikisha kwamba wamiliki wote wa viwanda vya ndani wanaajiri wazawa.
Dokta Magufuli ametoa agizo hilo leo Machi 11 mwaka huu
wakati alipokuwa akizindua kiwanda cha kufua vyuma cha Kahama Oil Mill kilichopo
mjini Kahama Mkoa wa Shinyanga.
Alisema kuwa wananchi wazawa ndio waliompigia kura, hivyo ni
lazima wapewe kipaumbele cha ajira katika viwanda hivyo.
“Kama wewe ni Waziri nimekuteua mimi, unaacha kuwaajiri
wazawa walionipigia kura unaenda kuchukua watu wa nje ya nchi hii haikubaliki”,
alisisitiza Dokta Magufuli.
Vilevile alitoa wito kwa mawaziri wote na wakurugenzi
wahakikishe kwamba, viwanda vinavyoanzishwa hapa nchini wanaoajiriwa kwanza ni
Watanzania.
Wamiliki wa viwanda wanapaswa pia kuhakikisha wanatumia
malighafi za ndani kwanza kutengeneza bidhaa badala ya kuagiza kutoka nje ya
nchi.
“Mwaka huu pamba nyingi imelimwa, kahama Oil Mill pia
mnatengeneza mafuta, hakuna haja ya kuagiza pamba kutoka nje wakati tuna pamba
ya kutosha hapa”, alisema.
Kuhusu kiwanda cha chuma Dokta Magufuli alisema malighafi inapatikana
nchini, hivyo iwapo Mkurugenzi wa Kahama Oil Mill anahitaji yupo tayari kumpa
bure badala ya kuagiza nje.
Pamoja na mambo mengine, amewataka Watanzania kuwa na mazoea
ya kununua bidhaa za ndani huku akiwataka wamiliki wa viwanda kutengeneza zenye
ubora ili kuhimili ushindani wa kibiashara.
No comments:
Post a Comment