Moja kati ya barabara za Manispaa ya Songea ya FFU Matogoro ambayo
inafanyiwa ukarabati.
|
Songea.
HATIMAYE Kampuni ya kimataifa ya Serikali
ya China, inayoitwa China Sichuan International Co-operation, kufikia Machi 25
mwaka huu itaanza rasmi ukarabati wa barabara za Manispaa ya Songea Mkoani
Ruvuma, kwa kiwango cha lami nzito.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya
Songea Mkoani humo, Mhandisi Samwel Sanya alisema hayo leo kuwa Kampuni hiyo tayari
imesaini mkataba baina yake na Halmashauri ya Manispaa hiyo.
Alifafanua kuwa mkataba unaonesha
kuwa, ukarabati wa barabara hizo zenye urefu wa kilometa 10.3 utaanza Machi 25
mwaka huu na unatarajia kukamilika Septemba 30 mwaka 2019.
“Mkataba ni wa miezi 18, fedha ambazo
zinatumika katika ukarabati huo ni bilioni 10.96, Mkandarasi wa sasa anaongeza
kilometa zaidi ya mbili, pia ataweka taa za barabarani”, alisema Sanya.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea
ilivunja Mkataba wa ujenzi wa lami nzito yenye urefu wa kilometa 8.6 kati yake
na Kampuni ya Lukolo yenye makao makuu yake jijini Dar es salaam, baada ya
Kampuni hiyo kukiuka masharti ya mkataba wa miaka miwili uliomalizika Juni 30 mwaka
2017.
Baada ya muda huo kumalizika Mkandarasi
huyo aliingizwa kwenye tozo (Liquidated Damage) kwa siku 100 ambapo Oktoba 8
mwaka jana ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo zilimalizika hivyo Manispaa
ilivunja mkataba rasmi na Kampuni hiyo ya Lukolo.
Pia kuvunjwa kwa mkataba huo, Manispaa
ya Songea ilianza mchakato wa kumtafuta Mkandarasi mwingine ambapo amepatikana
Mkandarasi wa Kampuni ya China Sichuan International, ambaye ataendeleza kazi
ya ukarabati barabara na kwamba Manispaa haijapata hasara yeyote baada ya
kuvunjwa kwa mkataba wa Mkandarasi wa kwanza.
Fedha za mradi huo ambazo ni zaidi ya
shilingi bilioni 14 zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango wa kuzijengea
uwezo Serikali za mitaa (ULGSP) mpango huo, unakusudia kuendeleza miundombinu
ya Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania Bara ikiwemo Manispaa ya
Songea.
Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi
2015 ulitarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka 2017 na kwamba Barabara za Manispaa hiyo
ambazo zipo kwenye mradi huu ni FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2, barabara
ya Songea Girl’s hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara ya
Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.
Barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda
yenye urefu wa kilometa moja, barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye
urefu wa kilometa 0.45.
No comments:
Post a Comment