Na Kassian Nyandindi,
Tunduru
MTU mmoja aliyejulikana kwa jina la Masudi
Namurumi (28) amefariki dunia, katika tukio la ajali ambayo ilihusisha Pikipiki
mbili kugongana uso kwa uso.
Mashuhuda wa tukio hilo walieleza
kuwa lilitokea katika eneo la makutano ya barabara iendayo kijiji
cha Nandembo na Kitalo Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma.
Pamoja na ajali hiyo kusababisha kifo
hicho, watu watatu wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo ambao walikuwa
abiria katika Pikipiki hizo.
Imeelezwa kuwa hali zao ni mbaya,
baada ya kupata majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo
walieleza kuwa tukio hilo lilitokea majira ya usiku na kwamba chanzo cha ajali
hiyo kimetokana na na mwendo kasi wa madereva wa Pikipiki hizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Gemini
Mushy amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akieleza kuwa Polisi bado
wanaendelea na uchunguzi.
Alisema kuwa wananchi ambao walishuhudia wakati hali hiyo inatokea walitorosha Pikipiki hizo na kwenda
kuzificha, katika maeneo yasiyojulikana ingawa hivi sasa tayari wamekwisha pata
kwanza namba ya Pikipiki ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Marehemu, Masudi.
Kamanda Mushy amewataka wananachi
ambao wanataarifa za eneo zilipofichwa Pikipiki hizo, watoe taarifa Polisi
ili ziweze kuchukuliwa kwa ajili ya taratibu za kisheria.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Rashid
Seif ambaye alikuwa dereva wa Pikipiki ya pili, Asiatu Peter na Ally Msokolo
ambao walikuwa abiria katika Pikipiki hiyo.
Mganga wa zamu Dokta Baraka Mmari, ambaye
ameufanyia uchunguzi mwili wa Marehemu huyo alisema kuwa chanzo cha kifo chake,
kimesababishwa na kupasuka kichwa baada ya ajali hiyo kutokea.
Akizungumzia hali za majeruhi hao, Dokta
Mmari alisema kuwa hali zao zinaendelea vizuri na kwamba maafisa tabibu,
wanaendelea na juhudi za kuwapatia matibabu ili kuweza kuokoa maisha yao.
No comments:
Post a Comment