Ugonjwa wa Nguruwe, unavyoteketeza Nguruwe Songea Mkoani Ruvuma. |
Songea.
KATIKA Manispaa ya Songea Mkoani
Ruvuma, wamesitisha uchinjaji wa Nguruwe katika maeneo yote ya Manispaa hiyo,
tangu mwezi Februari mwaka huu, kufuatia kuibuka kwa homa ya Nguruwe ambayo
haina kinga wala tiba.
Takwimu ambazo zimetolewa na Afisa
Mifugo na Uvuvi wa Manispaa ya Songea, Bilaly Mwegeni zinaonesha kuwa homa hiyo
ambayo inafahamika kwa jina la “African Swine Fever” katika kipindi cha kuanzia
Januari 31 hadi Machi 14 mwaka huu imeua Nguruwe 864.
Mwegeni alisema kuwa takwimu hizo za
vifo ni matukio ambayo yameripotiwa katika idara yake, ambapo uchunguzi umebaini
kuwa zaidi ya nusu ya Nguruwe waliopo katika Manispaa hiyo wamekufa kutokana na
ugonjwa huo, hali ambayo inahatarisha kuteketeza Nguruwe katika Manispaa hiyo.
“Takwimu zinaonesha kuwa Manispaa ya
Songea ina Nguruwe 4,581 tukifanya sensa ya idadi ya Nguruwe waliobakia katika
Manispaa yetu, naamini watakuwa hawazidi 2,000 kwa sababu kuna Nguruwe wengi
wamekufa na takwimu za vifo hazijaletwa hapa Ofisini kwangu”, alisema Mwegeni.
Pia Mwegeni alizitaja kata ambazo
zinaongoza kwa vifo vya Nguruwe hao kuwa ni Ndilima Litembo vifo (334),
Lizaboni (138), Msamala (90), Matarawe (66) na Ruhuwiko (34) na maeneo mengine
vifo vya Nguruwe huwa sio zaidi ya Nguruwe watano.
Kutokana na kuenea kwa homa hiyo Mkurugenzi
Mtendaji wa Manispaa ameagiza Watendaji wote wa Mitaa na Kata kuanzia sasa
wahakikishe hakuna mtu kuchinja, kuingiza au kusafirisha Nguruwe kutoka katika
maeneo mbalimbali.
Kadhalika uchunguzi uliofanywa na
mwandishi wetu umebaini kuwa homa hiyo ya Nguruwe ipo katika Halmashauri tatu
za Mkoa wa Ruvuma, ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Wilaya ya Songea
na Wilaya ya Nyasa.
Vilevile kutokana na hali hiyo Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa huo imeitisha mkutano wa wadau wa sekta ndogo ya Nguruwe, Machi
26 mwaka huu na kukutana nao kwenye ukumbi wa Maliasili mkoa kwa lengo la
kujadili mkakati wa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo na namna ya kudhibiti
ueneaji wake.
Ugonjwa huu wa Nguruwe kwa ujumla hauna
kinga na kwamba kitaalamu hauna madhara kwa binadamu ambapo kitaalamu Nguruwe
aliyekufa kwa ugonjwa huo anatakiwa kuzikwa katika shimo lililopuliziwa dawa ya
kuteketeza virusi lenye urefu wa zaidi ya meta moja.
No comments:
Post a Comment