Na Muhidin Amri,
Songea.
MKUU wa Majeshi ya ulinzi na usalama hapa nchini, Jenerali
Venance Mabeyo amewataka Watanzania kujiepusha na vitendo vinavyoweza kutishia
usalama wa nchi na kuharibu tunu ya amani tuliyonayo.
Aidha Jenerali Mabeyo, amewaomba Watanzania kuunga mkono
juhudi mbalimbali zinazofanywa na Rais Dokta John Magufuli dhidi ya wizi,
ufisadi na matumizi mabaya ya Ofisi za umma kwa kuwataja hadharani watu
wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Jenerali Mabeyo alitoa kauli hiyo juzi wakati akifunga maadhimisho
ya tamasha la Mashujaa wa Vita ya Majimaji lililofanyika kwenye viwanja vya
Makumbusho ya Mashujaa wa Vita hivyo mjini Songea.
Alisema kuwa mapambano ya vita dhidi ya wizi na ufisadi yaliyoanzishwa
na Rais Dokta Magufuli siyo ya mtu mmoja, bali kila Mtanzania anapaswa
kushiriki kikamilifu kwani mali zinazoibwa na baadhi ya Watanzania zinapaswa
kuwanufaisha watu wote.
Alifafanua kuwa kuna mambo yanayotishia usalama wa nchi yetu
na kwamba Serikali imedhamiria kuwatumikia wananchi wake kikamilifu, kwa
kuboresha huduma za kijamii na kutoa fursa ya kufanya kazi za kujiletea
maendeleo.
“Baadhi ya mambo yanayotishia usalama wa nchi yetu ni pamoja
na matumizi mabaya ya utandawazi ambayo mbali na kuharibu utamaduni wa nchi
yetu, watu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kuhamasisha
wananchi kufanya na kushiriki katika matukio ambayo yanaashiria uvunjifu wa
amani”, alisema.
Vilevile alishauri shule za msingi, sekondari na vyuo hapa
nchini kufundisha wanafunzi wetu umuhimu wa kulinda, kutunza amani pamoja na Watanzania
kuishi kwa kupendana badala ya kutumia muda wao kutafuta sababu za kutengana
ambazo hazina tija kwa taifa letu.
Katika hatua nyingine, Jenerali Mabeyo ameitaka Wizara ya
maliasili na utalii kuboresha makumbusho ya Mashujaa wa Vita ya majimaji ili yatumike
kwa ajili ya utalii, ambapo yanaweza kuliingizia taifa letu fedha nyingi.
Alisema kuwa makumbusho hayo ni muhimu kwani yatasaidia
kudumisha na kukumbusha historia ya nchi yetu na kuwataka Watanzania,
kuwaenzi kwa vitendo Mashujaa waliopigana vita hivyo kwa ajili ya kulikomboa
taifa letu kutoka mikononi mwa Wakoloni wa Kijerumani.
Kadhalika alisema Mashujaa wa majimaji walionesha uzalendo
mkubwa kwa taifa letu, kwa hiyo Watanzania waliobaki hawana budi nao kuonesha
kwa vitendo jinsi wanavyochukia vitendo vinavyoweza kudhoofisha kazi inayofanywa
na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dokta John Magufuli.
Siku ya makumbusho ya Mashujaa hao inawakumbusha Watanzania
namna Mashujaa walivyojitoa muhanga na kupoteza uhai wao kwa ajili ya wananchi wengine
na kwa manufaa ya nchi yetu.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Chiristine Mndeme alisema
Serikali ya Mkoa huo itahakikisha inaongeza nguvu katika kulinda mipaka yake
ili wananchi wa Mkoa huo, waweze kuendelea na kazi ya uzalishaji mali.
Mndeme alisema Serikali itasimamia na kulinda mali za Mkoa na
Taifa kwa ujumla kama walivyofanya Mashujaa hao ambao walikubali kupoteza
maisha yao kwa ajili ya nchi yetu.
Pamoja na mambo mengine, Mndeme ambaye pia ni Mwenyekiti wa
kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Ruvuma aliongeza kuwa kila mwaka
ifikapo Februari 27, Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Watanzania wanakutana
ili kuwakumbuka Mashujaa hao ambapo wataendelea kukumbukwa kwa faida ya vizazi
vya sasa na vijavyo.
No comments:
Post a Comment