Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
MWANAFUNZI wa darasa la saba, Shaibu Mpoto ambaye ni wa shule
ya Msingi Kichangani kata ya kichangani Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,
anashindwa kuendelea na masomo katika shule hiyo baada ya kuugua ugonjwa wa
kupooza miguu kwa muda mrefu.
Tatizo hilo ambalo limempata mwanafunzi huyo ni miaka minne
sasa imepita, lakini baada ya kupata msaada wa Baiskeli yenye magurudumu matatu
hivi sasa inamsaidia kwenda shuleni kuhudhuria vipindi vya masomo na kurudi
nyumbani kwake Kichangani ambako anaishi na ndugu zake.
Kampuni ya D&G Export Limited inayojishughulisha na kazi
ya ununuzi wa mazao na utunzaji wa Korosho Tunduru na Liwale Mkoa wa Lindi,
ndiyo ambayo imeweza kumpatia Baiskeli hiyo na kuondoa adha aliyokuwa akiipata
kwa muda mrefu mwanafunzi huyo.
Shaibu alikata tamaa katika kutimiza ndoto yake ya kuendelea
na masomo kikamilifu kutokana na kupata ugonjwa huo, ili hapo baadaye aweze
hata kujitegemea mwenyewe na kutoa mchango wake kwa Taifa hili.
Akizungumza jana na Mwandishi wetu alisema kuwa alianza
kupooza miguu yote miwili mwaka 2014 akiwa darasa la tatu, hivyo anashukuru kwa
kuweza kupata msaada huo.
Wakati mwingine ndugu zake Shaibu walikuwa wakilazimika
kumbeba mgongoni kumpeleka shule na kwamba baada ya kupata msaada huo imekuwa
ni mkombozi mkubwa kwao.
“Nashukuru kwa msaada huu ambao utanisaidia kwenda shuleni na
kurudi nyumbani, hata kwenda maeneo mengine bila kuhitaji kubebwa na mtu”,
alisema Shaibu.
Vilevile mlezi wa Shaibu ambaye ni Bibi yake, Fatma Kaluma
alisema kuwa hivi sasa ataweza kupata muda wa kupumzika kumbeba kila siku
asubuhi na jioni, na kuweza kufanya kazi nyingine za kujiongezea kipato
kutokana na hapo awali alishindwa kufanya hivyo kutokana na tatizo hilo la
mjukuu wake.
Fatma anawaomba Wasamaria wema waendelee kumsaidia mjukuu
wake, kwani hivi sasa anahitaji kupata sare za shule na vifaa vya masomo
darasani kama vile daftari, kalamu za kuandikia na vitabu vya kusoma.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo iliyotoa msaada huo, Geofrey
Kalamba alisema kuwa walikuwa wakiona huruma namna mwanafunzi huyo alivyokuwa
akikaa nyumbani kwa muda mrefu na kupata mateso ya kushindwa kuhudhuria kikamilifu
vipindi vya masomo darasani, hivyo waliona ni vyema sasa wampatie Baiskeli ambayo
wameinunua kwa gharama ya shilingi 320,000 ili iweze kumsaidia katika maisha
yake.
No comments:
Post a Comment