Na Kassian Nyandindi,
Madaba.
WAFUGAJI waliovamia katika hifadhi ya
Gesi Masowa, katika kijiji cha Kipingo kata ya Lituta Halmashauri ya Wilaya ya
Madaba Mkoani Ruvuma, wanatakiwa kuondoka mara moja kabla Serikali haijatumia
nguvu na kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa Wilaya
ya Songea, Pololet Mgema wakati alipokuwa akizungumza na Wawakilishi wa
wafugaji hao, Wenyeviti wa vijiji, Maafisa mifugo pamoja na viongozi wa Wilaya
ya Madaba.
Mgema alisema kuwa Serikali inayo
taarifa kuwa baadhi ya wafugaji wameingia katika jimbo la Madaba na kwenda moja
kwa moja katika hifadhi zilizotengwa kwa ajili ya makazi ya wanyama na kufanya
shughuli zao za ufuagaji, ambapo amewataka baada ya wiki moja kuanzia sasa wawe
wameondoka na kwenda katika ranchi ya Ngadinda iliyopo Wilayani humo ambayo
imetengwa na Wizara ya mifugo kwa ajili ya shughuli hizo za ufugaji.
Vilevile katika kipindi hicho alisisitiza
kuwa mifugo yote iwe imepigwa chapa ili kuzuia uingizaji holela wa ng’ombe,
kutoka maeneo mengine kwa kuwa kila Wilaya hapa nchini imekwisha tenga maeneo
ya wafugaji.
Kadhalika amewaonya Wenyeviti wa vijiji
kuhusiana na tabia ya kuwatoza fedha wafugaji, kwa kisingizio cha kuweka mpango
wa matumizi bora ya ardhi hasa kwa wafugaji wanaotoka nje ya Wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya amemuagiza Afisa
mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba pamoja na Watendaji wa vijiji vya
Lituta na Kipingo kwenda kwa wafugaji hao, ili kuangalia uwezekano wa kupata
njia ambayo itatumika kupitishia mifugo yao na kwenda katika ranchi ya Ngadinda
kwa ajili ya upigaji chapa ng’ombe wao bila kuharibu mazao ya wakulima wengine
mashambani.
Katika hatua nyingine, amemtaka
Mwenyekiti wa kijiji cha Kipingo kuacha mara moja tabia ya kukumbatia wafugaji
na kuwaingiza ndani ya hifadhi kwa lengo la kujinufaisha maslahi yake binafsi.
“Tunazo taarifa kuwa wewe Mwenyekiti
unahusika na uingizaji wa mifugo katika hifadhi ile kwa maslahi yako binafsi,
unawaambia wafugaji wasiondoke na wewe utawalinda nakushauri acha tabia hii
mara moja tutakushughulikia”, alisema Mgema.
No comments:
Post a Comment