Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme (aliyevaa kitambaa rangi ya njano) akipata maelezo mafupi kutoka kwa mjasiriamali juu ya faida ya ulaji wa matunda ya asili. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA kukuza maendeleo ya mwanamke,
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma imefanikiwa kusajili vikundi 50
vya wanawake ambao ni Wajasiriamali, wakiwa wanajishughulisha na biashara
ndogondogo.
Aidha vikundi hivyo vimekuwa
vikijishughulisha na shughuli za kilimo na ufugaji na kuweza kujipatia kipato
cha kuendeleza maisha yao.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na
Paschal Ndunguru ambaye ni Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii Wilayani humo, siku ya
maadhimisho ya wanawake duniani yaliyofanyika Wilayani hapa.
Alisema kuwa katika sehemu ya vikundi
hivyo, 18 vimefanikiwa kuanzisha SACCOS ya wanawake kwa lengo la kusimamia
utoaji mikopo na marejesho katika hali ya usawa ambapo ina jumla ya wanachama
300.
“Halmashauri yetu imefanikiwa kutoa
mikopo ya mzunguko kwa vikundi vya wanawake kumi, yenye jumla ya shilingi Milioni 10 ambazo zimetolewa kwa kupitia SACCOS hiyo kwa mujibu wa mwaka wa
fedha wa 2016/2017”, alisema Ndunguru.
Ndunguru alieleza pia kwa
kushirikiana na asasi mbalimbali zilizopo Wilayani Mbinga, wameweza kuendelea
kujenga uelewa kwa jamii juu ya haki ya mwanamke na mtoto wa kike hasa katika
mazingira ya vijijini na kwamba, kipindi cha mwaka 2016/2017 idadi ya viongozi
wapatao 53 wameweza kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
Hata hivyo kwa kushirikiana na wadau
wa maendeleo VETA na SIDO pamoja na asasi za kiraia Wilayani humo wameweka
vipaumbele vya kuwainua wanawake hasa waliopo vijijini, ambapo vikundi saba vya
wanawake ambavyo vimeanza kutekeleza dhamira ya Tanzania ya viwanda kwa
kujishughulisha na kazi ya usindikaji wa bidhaa na kuongeza thamani.
No comments:
Post a Comment