Na Muhidin Amri,
Tunduru.
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, umepokea jumla ya Shilingi
Bilioni 946,388,947.40 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopangwa
kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.
TASAF katika Wilaya hiyo hadi kufikia
mwezi Machi mwaka huu imeweza kutekeleza sehemu tatu ya mpango huu wa kunusuru
kaya maskini ambapo ni wa Uhawilishaji wa Fedha (CCT) kwa awamu 25 tangu
kuanzishwa kwake, Utekelezaji wa Miradi ya Ajira za Muda (PWP) kwa miaka
miwili, Ujenzi wa miundombinu ya Barabara pamoja na ujenzi wa zahanati ya
kijiji cha Tuwemacho.
Mratibu wa Mfuko huo Wilaya ya
Tunduru, Muhidin Shaibu alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi
wetu juu ya mapokezi ya fedha hizo.
Alisema kuwa mapokezi hayo hata hivyo
yameshuka ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi Bilioni 2.836,540,097.02 zilizopokelewa
na Mfuko huo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Shaibu alifafanua kuwa kati ya fedha
hizo Shilingi Milioni 408,600,000 zilitumika kuwalipa walengwa wa mpango wa
uhawilishaji wa fedha kwa kaya maskini (Conditional Cash Transfer - CTC) 13,856
zilizopo katika vijiji 88 Wilayani humo kwa kipindi cha mwezi Machi hadi Aprili
mwaka huu.
Katika kipindi hicho alisema Ofisi
yake pia ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 458,413,000 kutoka Serikalini kwa
ajili ya malipo ya kaya 13,450 ambazo zilishiriki katika shughuli za ajira za
muda, zilizotekelezwa katika kipindi cha hadi mwezi Disemba mwaka jana.
Alisema katika utekelezaji huo jumla
ya miradi 184 ikiwemo miradi 5 ya kudhibiti Makorongo, kutengeneza Mbolea ya
asili ipatayo 52, kuboresha visima 35 vya maji ya kunywa, upandaji wa miti
katika vyanzo vya maji, miti ya mbao na matunda katika mashamba 74 pamoja na
uanzishaji wa mabwawa ya samaki katika vijiji 10.
Alisema sambamba na miradi hiyo pia
fedha hizo zilitumika kwa ajili ya kuboresha mifereji yenye urefu wa kilometa 3
katika mradi mmoja wa shamba la umwagiliaji, kuboresha miradi mitatu ya
barabara za mitaa, kujenga mradi mmoja wa kivuko cha waenda kwa miguu na
kuchimba malambo ya kuhifadhi maji katika miradi mitatu.
Shaibu alisema TASAF huwapatia fedha
hizo kwa ajili ya kuwasaidia kupata huduma za afya, elimu na kupewa ruzuku ya
msingi ambayo huwawezesha kujiongezea kipato katika maisha yao ya kila
siku.
Katika utekelezaji huo aliongeza kuwa
pia kiasi cha Shilingi Milioni 28,263,590,000 sawa na asilimia 8.5 zilitumika
kwa ajili ya ukamilishaji wa shughuli za uwezeshaji katika ngazi ya Wilaya.
Alieleza kuwa kupitia utaratibu huo
pia ngazi ya kata walipata mgawo wa Shilingi Milioni 1,320,000 sawa na asilimia
1 na ngazi ya kijiji walipata Shilingi Milioni 8,800,000 sawa na asilimia 1.5
ambazo zilipangwa kwa ajili ya shughuli za uwezeshaji.
Sambamba na utekelezaji mradi huo pia
TASAF ilipokea Shilingi Milioni 74,079,274.40 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi
wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Tuwemacho.
Akizungumzia changamoto ambazo
wamekuwa wakizipata wakati wa ugawaji wa fedha hizo, Mratibu huyo alisema kuwa
licha ya elimu husika kutolewa kwa wanufaika hao bado jamii imekuwa na uelewa
mdogo juu ya miongozo na utendaji kazi wa mfuko huo wakati wa utekelezaji wa
miradi hiyo ya ujenzi.
Kwa mujibu wa maelezo yake alisema utekelezaji
wa mpango huo kwa ujumla unafuatia uzinduzi uliofanywa na Rais (Mstaafu) wa
awamu ya nne Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Agosti 15 mwaka
2012 na kuanza kutekelezwa mwaka 2013 ukilenga kunusuru kaya maskini, kwa
kuziwezesha kupata huduma muhimu hasa katika nyanja ya elimu, afya na maji.
Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii hapa
nchini, unatekelezwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao
huchangia wakiwemo Benki ya dunia, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweeden
(SIDA), Mpango wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Umoja wa
Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) pamoja na Shirika la Kazi la Umoja wa
Mataifa (ILO).
No comments:
Post a Comment