Na Mwandishi wetu,
Songea.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christine
Mndeme amewataka Vijana ambao wanajihusisha na biashara ya kuendesha Pikipiki
maarufu kwa jina la Bodaboda Mkoani humo kujiunga na mafunzo ya Mgambo ili waweze
kukabiliana na vitendo vya uhalifu, hasa wanavyofanyiwa na watu wenye nia mbaya
ambao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kuwanyang’anya Pikipiki zao ikiwa ndiyo
njia rahisi ya kutekeleza uhalifu wao.
Christine Mndeme. |
Mndeme alisema kuwa Serikali ya Mkoa itahakikisha
kwamba inatoa mafunzo ya mgambo kwa vijana wote watakaokuwa tayari, ili kuweza kuwapata
vijana wengi ambao watakuwa na mchango mkubwa katika masuala ya ulinzi na
usalama ndani ya Mkoa na nchi kwa ujumla.
Alitoa kauli hiyo jana akiwa katika
uwanja wa michezo wa Majimaji mjini Songea, wakati alipokutana na kuzungumza na
vijana hao zaidi ya 200 waendesha Bodaboda kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa
ya Songea, huku akiwataka waachane na tabia ya ulevi na matendo maovu ambayo
hayafai katika jamii.
Kadhalika aliwaeleza vijana hao
waunge mkono, jitihada zinazofanywa na Rais Dokta John Pombe Magufuli katika
kuhakikisha wanapiga vita vitendo vya wizi wa mali za umma, ufisadi na matumizi
mabaya ya madaraka.
Katika hatua nyingine Mndeme amewataka
pia waunde umoja wao na kuusajili kisheria, utakaoweza kuwasaidia kuwa na nguvu
moja hasa katika shida na raha huku akiahidi kuwachangia shilingi Milioni 1
katika umoja huo ili waweze kufungua akaunti ya akiba benki.
Alisema kuwa kazi ya kuendesha
Bodaboda ni kazi halali inayowapatia kipato cha kila siku, kama ilivyokuwa kazi
nyingine hivyo vizuri wakajitambua na kupendana na sio kubaguana.
No comments:
Post a Comment