Kahawa ambayo ipo shambani kama hii, ikikosa pembejeo za kilimo kama vile madawa na mbolea huwa kama hivi baada ya kukosa virutubisho halisi na kushambuliwa na wadudu waharibifu. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya Wakulima wanaozalisha zao
la Kahawa Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wamesema kwamba hivi sasa wanashindwa
kuendesha kilimo cha zao hilo kutokana na mfumo uliowekwa na Serikali wa vyama
vya ushirika, kushindwa kuwakopesha pembejeo za kilimo wakulima hao kama vile
madawa na mbolea.
Aidha kwa nyakati tofauti walisema
kuwa ni vyema wakati Serikali inajipanga kutekeleza hilo, wangeruhusu kwanza Makampuni
binafsi ambayo yalikuwa yakiwawezesha pembejeo hizo yangeendelea kusambaza kwa
wakulima hao, huku wakisubiri mfumo wa ushirika ukiendelea kuimarishwa.
Walidai kuwa mfumo wa vyama vya
ushirika sio kwamba wanaupinga, lakini imekuwa ni haraka mno kuyasitisha
Makampuni hayo ambayo yalikuwa ni msaada mkubwa kwao, hivyo ni vyema ungetolewa
muda kwanza na masharti kadhaa namna ya kuweza kusaidia wakulima hao.
“Hivi sasa imekuwa ni tatizo kwetu
tunashindwa kununua pembejeo za kilimo kama vile mbolea na madawa ya kupuliza
kwenye mashamba yetu, tulikuwa tunaiomba Serikali ingetupatia muda kwanza
wakati inajipanga na utekelezaji wa jambo hili”, walisema wakulima hao.
Pia zaidi ya asilimia 60 ya wakulima
wa kahawa Wilayani Mbinga, wengi wao wanaiomba Serikali ingeweza kulegeza
kwanza masharti iliyoweka sasa, ili makampuni hayo yaweze kuwakopesha pembejeo
hizo na kunusuru mazao yaliyopo kwenye mashamba yao yasiweze kuendelea kuathirika
na magonjwa mbalimbali.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa
habari hizi kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari wakiwemo wataalamu wa
kilimo ndani ya Wilaya hiyo, nao wameeleza kuwa katika kipindi cha msimu wa
mwaka huu vyama vya ushirika havitakuwa na uwezo wa kukopesha pembejeo hizo
wakulima hao wa kahawa.
Walisema Serikali katika kipindi hiki
inajipanga kwanza namna gani ya kuboresha vyama hivyo, ili hapo baadaye kuanzia
mwakani ushirika uweze kuanza kujitegemea wenyewe namna ya kusaidia wakulima
hao.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Cosmas Nshenye
alipoulizwa juu ya hali hiyo alisema kuwa wanajipanga kutoa elimu kwa viongozi
wa vyama vya ushirika ili waone ni namna gani viongozi hao wataweza kuhudumia
wakulima.
Nshenye alipotakiwa kutolea ufafanuzi
juu ya malalamiko ya wakulima hao kukosa pembejeo katika msimu huu alibainisha
kuwa taratibu husika zitakapokuwa tayari, Halmashauri kwa kushirikiana na vyama
hivyo vya ushirika vilivyopo Wilayani hapa wataweza kusaidia wakulima kwa
kuwakopesha pembejeo za kilimo za zao hilo la kahawa.
“Tunajua ni kweli baadhi ya wakulima
hawana uwezo wa kuhudumia mashamba yao, lakini ni lazima viongozi hawa wa vyama
vya ushirika na wataalamu wa kilimo wajipange kwanza kuhudumia wakulima”,
alisema Nshenye.
No comments:
Post a Comment