Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amesema kwamba kuendelea kutokea kwa tatizo la mlipuko wa ugonjwa wa
kipindupindu mpaka sasa katika kata ya Ukata, Litembo na Matiri kunasababishwa
na wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo kutozingatia masuala ya usafi.
Cosmas Nshenye. |
Aidha alieleza kuwa hali hiyo ya uchafu inatokana pia na
Watendaji wa vijiji na kata hawatimizi majukumu yao ya kazi ipasavyo, ikiwemo
kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuzingatia kanuni za usafi majumbani
mwao.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu huyo wa Wilaya wakati alipokuwa
akizungumza na viongozi mbalimbali wa Wilaya hiyo, kwenye kikao cha tathimini
ya elimu katika ukumbi wa Jimbo la Mbinga uliopo mjini hapa.
Nshenye alisema kuwa kufuatia uzembe huo unaofanywa huko
umesababisha kutokea kwa vifo vya watu watatu, ambao wamefariki dunia kwa
kipindupindu kwa nyakati tofauti tokea ugonjwa huo ulipoanza kujitokeza Januari
29 mwaka huu kwenye maeneo hayo.
Alisisitiza kuwa Watendaji hao wanapaswa kutumia nguvu katika
kuwaelimisha wananchi hao ili taatizo hilo lisiweze kuendelea kuleta madhara na
kwa yule anayekaidi achukuliwe hatua za kisheria.
“Serikali tumekuwa tukitumia gharama kubwa kupambana na
ugonjwa huu lakini kama Watendaji wa vijiji na kata, mngesimamia ipasavyo watu
wazingatie usafi katika maeneo yao wanayoishi hakika ugonjwa huu usingeweza
kuendelea kusumbua, wakufanya kipindupindu kiishe ni sisi viongozi kutimiza
majukumu yetu ya kazi ipasavyo”, alisema Nshenye.
Pia alisema kuwa badala yake Watendaji hao wamekuwa
wakiwaachia Wahudumu wa afya peke yao wakihangaika namna ya kudhibiti ugonjwa
huo, hivyo aliongeza kuwa kwa mtendaji ambaye anaona hataki kufanya kazi au
kutekeleza majukumu aliyopewa na Serikali ni vyema aachie ngazi mapema kabla
hajachukuliwa hatua za kinidhamu.
“Na mimi nisingependa tuishi kwa msuguano kila mmoja
ajitathimini utendaji wake wa kazi, tuache kufanya kazi kwa mazoea”,
alisisitiza.
Katika hatua nyingine alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito kuhakikisha kuwa Waganga wote
wa jadi wawe wamesajiliwa na kutambuliwa kisheria.
Nshenye alimpatia mwezi mmoja Mkurugenzi huyo ahakikishe
amekamilisha kazi hiyo na kumpelekea Ofisini kwake idadi kamili ya Waganga hao
waliopo Wilayani humo.
“Ukishapata idadi yao niletee Ofisini kwangu, ili niweze
kuwatambua ni wangapi wana kibali na wale wasiokuwa na kibali”, alisema.
No comments:
Post a Comment