Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa katika shule za
Sekondari zilizopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Wanafunzi 60 wa kike wanaosoma
katika shule hizo wameshindwa kuendelea na masomo mwaka jana 2017 kutokana na kuwa
na ujauzito.
Wazazi, walezi na jamii ndiyo
wamenyoshewa kidole katika suala zima la malezi ya watoto wa kike, ambapo
wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha hata pale mtoto huyo anapokuwa amepata
ujauzito hususan Serikali inapotaka kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa
wanaohusika na tatizo hilo.
Joseph Kapere ambaye ni Afisa elimu
Sekondari wa Wilaya hiyo alisema hayo hivi karibuni, wakati alipokuwa akizungumza
kwenye kikao cha tathimini ya elimu kilichofanyika mjini hapa.
Kufuatia hali hiyo imeelezwa kuwa kwa
kiasi kikubwa imekuwa ikichangia watoto hao kukatisha masomo yao.
Baadhi ya wadau wa elimu katika
Wilaya hiyo, wamependekeza kuwa mwanaume yeyote atakayepatikana na kosa la kumpa
mimba mwanafunzi, apewe adhabu ya kifungo cha maisha badala ya sheria ya sasa
ya kifungo cha miaka 30.
Adelgot Milinga Afisa Mtendaji wa
kata ya Litumbandyosi alisema kwamba iwapo Serikali itaongeza adhabu kwa watu
hao itasaidia kupunguza tatizo hil kwa wanafunzi na watoto wadogo chini ya umri
wa miaka 18 ambalo linao onekana kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Alieleza kuwa kifungo cha miaka
30 bado hakioneshi kama ni suluhisho la kuweza kumaliza tatizo la mimba
kwa wanafunzi wa kike ndani ya Wilaya hiyo na hata katika Mikoa mingine hapa
nchini hivyo Serikali iangalie namna kuongeza adhabu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Mbinga, Cosmas Nshenye alisema hadi sasa ni asilimia 90 ya watoto ambao walioandikishwa
kuanza elimu ya msingi Wilayani humo katika kipindi cha mwaka huu na wale
waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza ndiyo wanaotakiwa kuripoti katika shule
walizopangiwa.
Kutokana na tatizo hilo, ameagiza hadi
kufikia tarehe 30 mwezi huu watoto wote waliopo majumbani ambao wazazi bado
hawajawapeleka shule, wahakikishe wanakwenda shule kabla ya kuanza msako
kabambe wa kufuatilia watoto na wazazi wao.
Nshenye alisema ni aibu kubwa kuona Wilaya hiyo imeshuka kitaaluma kwa kushika nafasi ya 137 katika matokeo ya
darasa la saba mwaka 2017 kutoka nafasi ya 127 katika matokeo ya mwaka 2016.
Amewataka wadau wa elimu kutafuta
majawabu ya kumaliza tatizo hilo mapema huku akiwaagiza Watendaji wa vijiji na
kata kuhakikisha kwamba wanashirikiana na vyombo vingine vya sheria vya
Serikali kuwasaka watoto na wazazi wao.
No comments:
Post a Comment