Na Kassian Nyandindi,
SIKU zote binadamu anapozungumzia
jambo la kimaendeleo kuelekea Uhuru wa Tanganyika, amekuwa akitoa taswira au
picha ya mchango wa watu mbalimbali ambao wamefanya kazi hiyo, hadi kufikia
kilele cha mafanikio ambapo ndani yake wapo wanasiasa na jamii ya kawaida ambao
walivuma na wengine wasiovuma.
Aidha katika kundi hilo wapo wake kwa
waume, wametangulia mbele ya haki ambao ni wengi na wachache ndiyo waliobaki
ambapo kwa maana hiyo, wapo Waasisi wa siasa ya nchi hususan katika chama chetu
cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho ndicho kimebeba chimbuko
la Uhuru na maendeleo ya Tanganyika na baadaye tukaipata Tanzania.
Katika makala haya mmoja wa hao yupo
Mzee Costantine Oswald Millinga (96) huyu ni Mwanasiasa mkongwe na Mtanzania,
mwenye historia ndefu katika kuasisi vyama vya Tanganyika African Association
(TAA) na Tanganyika African National Union (TANU) akiwa mkazi wa baadhi ya miji
iliyokuwa nguzo za vyama hivyo hapa nchini.
Mvuto huo ndiyo uliomfanya Rais
mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokuwa madarakani, kumualika Mzee
Millinga kuwa mmoja wa watu katika uzinduzi wa sherehe ya miaka 50 ya Uhuru
zilizofanyika kwenye viwanja vya Mnazi mmoja, jijini Dar es salaam mwezi Julai
mwaka 2011 na akawa kivutio kikubwa.
Mzee Millinga alionesha kuwa na uwezo
mkubwa na kumbukumbu ya kusimulia kwa ufasaha historia ya TAA na TANU licha ya
umri wake kuwa mkubwa, huku akiibua mambo ambayo wengi wao hawakuyajua au
hayapo katika maandishi ya historia.
Katika vyama vyote vya TAA na TANU
Mzee huyo anayo “mikono yake” ambapo safari hiyo ilianza katika simulizi ya
mwaka 1952 akiwa mjini Ngudu Wilayani Kwimba, Mwanza kwa baba yake mdogo
aliyekuwa Inspekta wa Polisi ambaye alikuwa akifanya mipango ajiunge na Shirika
la Posta.
Hapo walitembelewa na rafiki wa baba
yake mdogo alitokea mjini Masasi, Mtwara aliyemtambua kwa jina la Frederick
Mchauro ambapo mgeni huyu alikuja na mawazo ya kumshawishi aachane na kazi za
Posta na badala yake ajiunge na ajira ya Ofisi ya Maendeleo ya Jamii huko
Masasi.
Pamoja na mambo mengine, baadaye
kulikuwepo mawazo mbadala ambapo alipata ajira hiyo mjini Tabora wakati huo
kukiwa na vuguvugu kubwa la mchakato wa kuanzishwa kwa TAA, kikiwa ndiyo chama
kilichojumuisha Wakulima na Wafanyakazi wazalendo.
Pia Mzee Millinga anamkumbuka
kiongozi wake wa kazi kwa wakati huo aliyemtaja kwa jina la Leonard Kunambi,
ambaye huyu alimshawishi kujiunga na TAA lakini ndani ya kipindi kifupi mchango
wake uliwavutia wanachama wengine hata akachaguliwa kuwa Katibu.
Hapo ndipo mwanzo wa ushiriki wake
kikamilifu wa Mzee huyu katika siasa ulipoanza wakati huo akiwa kijana mwenye
umri wa miaka 26 tu, katika zama hizo kasi ya kujijenga na TAA ilipamba moto
mjini Dar es Salaam, Tabora na maeneo mengine hapa nchini.
Joto la siasa kwa Watanganyika kutaka
haki ya kujitawala wakati huo lilikuwa juu, wakati TAA ikilenga kudai usawa
kati ya jamii ya Waasia, Wazungu na Waafrika.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida
jambo hili liliwakera Serikali ya Kikoloni ya Mwingereza chini ya Gavana Edward
Twining huku Wakoloni hao wakikerwa na msukumo huo wa Waafrika na kusababisha
kupiga marufuku wafanyakazi wa Serikali kushiriki siasa za chama cha TAA.
Mzee Millinga akiwa Tabora waliandika
barua kwa Serikali ya kikoloni wakitaka watumishi wa Serikali waendelee
kushiriki katika siasa za chama hicho na kwamba ombi hilo lilikubaliwa kwa
kupewa miezi sita ikiwa ni kipindi cha angalizo.
Kufikia mwaka 1953 alifahamishwa na
Mwenyekiti wake aliyemtaja kwa jina la Mwalimu Said Haroub, kwamba
wangetembelewa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni kiongozi mkubwa wa
TAA kutoka Dar es Salaam ikiwa ni muda mfupi tu tangu aliporejea kutoka
masomoni, Chuo kikuu cha Edinburg Uingereza.
Mwalimu Haroub alikuwa akifundisha
katika Sekondari ya Tabora na huko nyuma alikwisha mfundisha Mwalimu Nyerere
katika shule hiyo.
Mzee huyo anataja wajumbe wengine wa
Kamati ya TAA huko Tabora kuwa ni pamoja na Walimu wa shule hiyo ya Tabora ambao
ni Stephen Mhando na Erasto Mangenya.
Wengine ni Mshairi maarufu, Abdul
Saadan Kandoro, Sheikh Amri Abeid Kaluta anayetajwa na Mzee Millinga kwamba
“alikuwa maarufu sana” na Sheikh Abdallah Kivuruga ambaye anamtaja alikuwa “alwatani
wa mjini”.
Mwingine katika safu hiyo ni Germanus
Pacha aliyekuwa mtendaji mkuu wa Baraza la Machifu Tabora na mwanasiasa
aliyejulikana baadaye, Balozi Tebandebage.
Wakati huo kwamba Mwalimu Nyerere
alifika na kuwahutubia, hata hivyo katika kufunga kikao Mwenyekiti wa TAA Tabora
alitamka kwamba “ndicho kikao cha mwisho cha Katibu” yaani Mzee Millinga
anahama.
Mwalimu Nyerere akauliza anakwenda
wapi?, ambapo Mzee Millinga katika tukio hilo ambalo ilikuwa mara ya kwanza
kwake kuonana ana kwa ana na Nyerere, ambapo Nyerere alijibiwa kwamba Katibu
(Millinga) anahamishiwa Dar es Salaam.
Mzee Millinga alipoingia Dar es Salaam
Mzee huyu wakati anasoma Januari
mwaka 1954, tayari alikwisha ripoti jijini Dar es Salaam, kituo chake cha kazi
kikiwa katika idara ya Maendeleo ya Jamii jengo la Arnatoglu, akiwajibika chini
ya kiongozi wake aliyemtaja kwa jina la Denice Ombea.
Anasema Mwalimu Nyerere alikuwa na
kawaida ya kufika mjini Dara es Salaam mara kwa mara akitokea Pugu hasa kwa
siku za Jumamosi na kwamba walipokutana na Nyerere jirani na jengo hilo Dar es
Salaam alimtamkia kwamba; “Millinga umekuja, nilivutiwa sana na maneno aliyoyasema
Mwenyekiti wa (TAA-Tabora) juu yako”. Hapo Mzee Millinga alimjibu akisema; “na
mimi nasema chama ni hicho hicho”.
Jambo hilo walikubaliana na Mwalimu
Nyerere aliyemuahidi kwamba atawashawishi wenzake wamuingize katika Kamati ya
TAA Dar es Salaam na hatimaye walikubali, katika hali ambayo Mzee huyu anasema
ndivyo alivyoingia katika Kamati hiyo.
Katika vikao vyao vya TAA Mkoa wa Dar
es Salaam, walianza kujenga hoja ya kuibadili ili iwe na sura ya kisiasa kwa kuwa
iliyokuwapo haikuwa na nguvu na waliafikiana kufanya hivyo.
Vilevile mjadala ulikuwa mkali na
walitaka kuondoa neno “Association” katika jina la chama hicho, hiyo
ilimaanisha Ushirika jambo ambalo waliona waachane nalo na kukipatia jina la
“Union” ikimaanisha “Umoja” wakiamini lina ushirikishaji wa wengi.
Kwa maana hiyo walipata pendekezo
katika kikao chao cha TAA kwamba chama kiitwe Tanganyika African Union (TANU)
na hasa neno Union liliwekwa kwa nia ya kujumuisha watu wote, lakini hilo
wakalitafakari na waliona kwamba kwa kuwa nchi ya Kenya kuna Kenya African
Union (KAU) chini ya Jomo Kenyatta, iliyopingwa marufuku na Uganda ambapo
kulikuwepo Uganda African Congress (UAC) ikizingatiwa kwamba maeneo hayo
kulikuwa na makoloni ya Mwingereza.
Hatua hiyo ilifanya Wajumbe wa TAA
wagawanyike kwa makundi ya kanda, ambapo kila kundi walikuwa wakitafakari ni
jina gani linafaa kwa ajili ya kuanzisha chama kipya cha siasa.
Kanda hizo ni Mashariki yaani Dar es
Salaam, Pwani na Morogoro na kwamba Magharibi kulikuwa na Kigoma, Tabora na
Mpanda huku kukiwa na kanda ya Mwanza na Bukoba pamoja na ya Kaskazini yaani
Arusha na Moshi.
Wakati huo waliokuja na wazo la TANU
ni wenzetu wa kutoka Mwanza ambao ni akina Saddan Kandoro, Lameck Makaranga na
Walter Bugoke au kwa jina lingine maarufu alikuwa anaitwa “Kenyatta wa
Tanganyika”.
Mnamo mwaka 1954 hapo ndipo Chama cha
TANU kilizaliwa na kuandikishwa rasmi ikiwa ni chama kipya cha kisiasa kuchukua
nafasi ya TAA.
Wakati huo, Serikali ya Kikoloni
ilipiga marufuku watumishi wa Serikali (Umma) kushiriki kwenye masuala ya
siasa, jambo ambalo lililomfanya aendelee kushiriki katika mikutano ya siasa za
TANU kwa siri bila kuwa na kadi ya chama ili kuweza kulinda ajira yake, tofauti
na wana – TANU wengine waliokuwa katika ajira ya Serikali kama vile Mwalimu
Nyerere wao waliamua kujitosa kikamilifu na kuwa huru katika shughuli za chama.
Lakini maisha ya Mzee Millinga
binafsi nimebaini yana mengi katika siasa za nchi na utumishi wa umma kwa
ujumla, ikiwemo kujenga urafiki mkubwa na wanasiasa waandamizi nchini kama vile
Hayati Rashid Kawawa.
Mzee huyo alifikia hatua ya kujikita katika
masuala ya siasa na utumishi baada ya kupitia uzoefu muda mrefu wa kusaka
maisha hadi Ughaibuni yenye simulizi na vitimbi vingi baada ya kukerwa na mfumo
wa uongozi wa kikoloni nchini.
Mbali na kushiriki siasa hasa katika
harakati za kuanzisha TAA na TANU pia ni kinara katika utumishi wa umma ambapo
baada ya Uhuru amekuwa katika idara ya Maendeleo ya Jamii hadi alipostaafu
akiwa mzoefu hasa.
Baada ya Uhuru alikuwa daima mkimya
kuhusiana na masuala ya siasa huku akijikita zaidi katika utumishi wa umma
ingawa mapenzi yake makubwa kwa TANU hakuweza kuyaweka pembeni, aliyaweka rasmi
alipojiunga na chama hicho kwa kukata kadi baada ya Uhuru ambapo huko nyuma
alihofia angeachishwa kazi na Serikali ya kikoloni ambayo ilipiga marufuku
watumishi wote wa umma kushiriki siasa.
Tangu zama hizo alikuwa pia ni rafiki
wa karibu wa Muasisi wa Taifa la Tanganyika, Kleist Sykes na vilevile ni rafiki
wa karibu wa hayati Mzee Rashid Mfaume Kawawa.
Tunamkumbuka Kawawa alivyoshiriki
katika harakati za Uhuru wa Tanganyika kwa namna mbalimbali.
Wasifu kama huo na mengi umemfanya
Mzee Millinga awe mtu anayeheshimika miongoni mwa wanaomfahamu, hasa kwa hulka
yake ni vigumu kujikweza na ndilo jambo linalomfanya asifahamike.
Miongoni mwa wanaomtambua na
kumheshimu kwa hadhi anayostahili ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kanali
Mstaafu Edmund Mjengwa ambaye amekuwa akimtambua kwa staili ya kipekee kwenye
shughuli muhimu za kitaifa ambapo huwa hakosi kufanya hivyo.
Hilo ndilo lililotokea wakati Rais Jakaya
Kikwete alipozuru Wilayani Mbinga June 4 mwaka 2011 katika sherehe ya kumtawaza
Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Mbinga John Ndimbo ambapo alikuwa miongoni
mwa wazee waalikwa wakibadilishana mawazo na Rais Kikwete.
Mazungumzo hayo yaliweza kumuongezea
elimu ya ziada Rais Kikwete juu ya mengi kuhusu maisha binafsi ya hayati Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, tangu zama hizo akiishi Magomeni, Dar es
Salaam.
Kumbe kumtambua ni Muasisi wa TANU,
suala hilo lilimgusa Rais Kikwete na hata kuagiza uongozi wa chama kufanya
utaratibu wa kuhakikisha kwamba anakuwa miongoni mwa wageni rasmi wa kuzindua
sherehe za miaka 50 ya Uhuru iliyofanyika Julai 7 mwaka 2011, na kwamba bila
kujua kinachoendelea alipewa taarifa na uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na wa
Mkoa wa Ruvuma walimsafirisha hadi Dar es Salaam.
Kuhusu mchakato wa Uhuru
Mzee Millinga ana mengi kuhusu
kipindi hicho, wakati huo Kawawa akiwa tayari ni Katibu Mkuu na mwanaharakati
mwandamizi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TFL).
Wakati huo vuguvugu la TANU
iliyoshirikiana kwa karibu na TFL mwaka 1958 katika uchaguzi mkuu ulitokea
mgogoro mkubwa, juu ya ama TANU ikubali kushiriki au wakati huo Serikali ya
kikoloni ilikuja na hoja kwamba uchaguzi utafanyika kwa utaratibu wa kura tatu
ambazo ni za Mzungu, Mhindi na Mwafrika.
Mwalimu Nyerere alifanya jitihada ya
kuwashawishi wana – TANU wakubali hoja hii kwa kutumia mkutano uliofanyika
Tabora ulioongozwa na Sheikh Kihore, lakini wanachama wengine kama Bwana Zuberi
Mtemvu hakukubaliana na hoja hiyo na wakati wa uchaguzi alijitoa TANU na
kuanzisha chama kilichoitwa UTP.
Wakati huohuo wapo watu wengine
waliosimama kama wagombea binafsi na walifanikiwa kama vile Chifu Amri Dodo wa
Mbulu na Chifu Herman Sarawati wa Babati.
Walikuwepo pia wahindi walioshiriki
uchaguzi wa kuiunga mkono TANU kama vile Bwana Karimjee Jivanjee na Amir Jamal,
Mzungu Dereck Bryceson aliiunga mkono TANU na kwamba katika uchaguzi huo TANU
iling’ara kwa kuwa hata wale waliosimama kama wagombea binafsi walikiunga
mkono.
Licha ya upoinzani uliojitokeza hoja
ya mwalimu Nyerere ilionekana ni ya msingi, kwani TANU iliibuka kinara na kuwa
na hadhi ya kupewa haki ya kuongoza nchi.
Itakumbukwa kuwa baada ya Vita Kuu ya
Pili ya Dunia, Tanganyika ilikabidhiwa kwa wakoloni wa Kiingereza kutoka kwa
Wajerumani kwa udhamini hadi itakapopata uwezo wa kujitawala.
Katika harakati hizi Mzee Millinga na
wadau wengine muhimu wa Uhuru wa Tanganyika, John Rupia ambaye aliweza kutoa
mchango wake wa shilingi 14,000 katika kumfahamisha safari hiyo ya Mwalimu
Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa.
Ambapo wakati huo wakoloni waliweza
kuwakatisha tamaa jamii ya Wamisionari na walitumia nafasi zao kuwakejeli
Watanganyika kuwa bado hawakuwa na uwezo wa kujitawala, lakini ndoto ya
Watanganyika ilitekelezwa Disemba 9 mwaka 1961.
Maisha ya Mzee Millinga
Mzee huyu alizaliwa Novemba 22 mwaka
1921 akiwa mtoto wa kwanza wa Mzee Oswald Millinga na mama yake Victoria katika
kijiji cha Nkaya, Kata ya Lituhi Wilaya ya Nyasa (Zamani Mbinga) Mkoani Ruvuma.
Yeye ni mzaliwa wa kwanza katika uzao
wa watoto watatu, baba yake alikuwa fundi cherehani na mdogo wake mmoja
alifariki dunia angali mdogo. Dada ya Mzee Millinga ana umri wa miaka 93.
Mzee Millinga alianza masomo mwaka
1926 katika shule ya msingi Nkaya kuanzia ya awali na baadae shule ya msingi
hadi darasa la nne, alisoma palepale kijijini kwao Nkaya.
Baadae aliendelea na masomo ya darasa
maalum la Kiingereza kwa miaka miwili katika shule ya Mision Peramiho.
Mwaka 1936 hadi mwaka 1938 alipata
mafunzo ya ualimu hapo hapo Mision ya Peramiho ilivyokuwa chini ya Wajerumani.
Alipohitimu, alianza kazi ya
kufundisha katika shule ya maalum iliyokuwepo pale Mision Peramiho katika
Seminari ya Kikatoliki ya Peramiho, akiwa hapo aliingia katika mgogoro na Mkuu
wa shule ambaye alimtuhumu kuwa hafuati amri ya uongozi ya kukata nywele kila
baada ya wiki mbili, ambapo Mzee huyu wakati wote alikuwa mtanashati na wakati
huo alipenda kuchana nywele kwa mtindo wa “Way”.
Mgogoro huu ulisababishwa asimamishwe
kazi kwa muda na kisha akahamishiwa kufundisha katika shule ya Nkaya
alikosomea, aliweza kufundisha katika shule hiyo mpaka yalipotokea manyanyaso
mengine ya kikoloni, ambapo Mwalimu Mkuu alimkera baada ya kumtukana mbele ya
Wanafunzi na kumchapa makofi.
Sakata hilo liliamuliwa na Mkaguzi wa
elimu kutoka Peramiho ambaye katika uamuzi wake alimhamishia katika kata ya
Lituhi, jirani na Ziwa Nyasa ambako kulikuwa ni maili mbili kutoka alikokuwa
huko alifanya kazi kwa mwaka mmoja na akaamua kuacha.
Mwaka 1942 Mzee Millinga aliibuka na
uamuzi mwingine wa kuachana na kazi ya ualimu na akaamua kufanya safari ya
kwenda Afrika Kusini kutafuta kazi, wakati huo nchi hiyo ilikuwa chini ya
utawala wa Makaburu.
Alivyoianza safari ya kwenda huko
akiwa na wenzake watatu, alikusanya nguo zake akizitaja kuwa ni Kaptura ya
ziada (Mtindo wa vijana wakati huo ilikuwa kuvaa Kaptura) shati na shuka.
Wakati huo walipanda Mtumbwi, kutoka
ukingoni mwa Ziwa Nyasa na waliweza kusafiri hadi Kyela na kisha wakaenda mji
wa Karonga walikopanda meli ya MV Mpasa kwa nauli ya shilingi 30 wakati huo,
mpaka Nkhata Bay na baadae walipanda gari Moshi hadi mji mkuu wa Blantyre.
Baada ya hapo safari iliendelea kwa
gari Moshi kupitia Msumbiji na kuendelea hadi Zimbabwe, walipofika katika mji
wa Salisbury wakiwa katika gari Moshi walikamatwa na askari waliowahoji kuhusu
vibali vyao vya kusafiria.
Pamoja na mambo mengine, wakati huo
walisafiria kwa kutumia nyaraka walizozitayarisha kwa maarifa yao zilizofanana
na hati za kusafiria za wakati huo, lakini askari wale hawakuwaamini hivyo
waliwekwa mahabusu na kuwafungulia mashitaka.
Wakiwa mahabusu walikutana na baadhi
ya askari waliotokea Tanganyika ambao waliwasaidia kwa kuwaelekeza kwamba, ili
wajinasue wajifanye hawajui Kiingereza wala Kiswahili bali wazungumze lugha ya
Kimanda tu.
Mbinu hiyo ilileta utata mkubwa
walipopelekwa Mahakamani, ilibidi Hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi yao atafute
mwendesha mashitaka anayejua Kiswahili ambapo pia iligundulika kuwa hawakijui
Kiswahili.
Hivyo Mahakama iliwapa kibali cha
kuwepo Zimbabwe kwa siku 14, waliishi huko wakihifadhiwa na Watanganyika wenzao
na baadae waliendelea na safari ya kwenda Afrika Kusini, safari iliyowachukua
siku tano huku wakivuka mbuga ya Transvaal kwa mguu wakiwa kundi la watu
wapatao 10 walikabiliana na wanyama wakali na ukosefu wa maji ya kunywa, kuna
wakati hawakulala huku baadhi ya maeneo walipofika walikuwa wakipeana zamu pale
walipotaka kulala wengine wanakuwa macho wakijilinda na kukoka moto, kitu cha
kustaajabisha ni kwamba baadhi ya wanyama wakali kama vile Faru waliuzunguka
moto huo.
Walilazimika kuingia kwenye mashimo
yaliyochimbwa na wanyama kutafuta maji, wakati mwingine walikuwa wakifukua
mabonde ya mito ili kuweza kupata maji hatimaye safari yao ilifika katika mgodi
wa Transvaal, ambako alienda kuomba kazi na akabahatika kupangwa katika stoo ya
vyombo vya kuchimbia mgodi wa madini.
Alipewa kazi hiyo kutokana na kuwa na
mwandiko mzuri na wenzake walipata kazi katika vitengo vingine vya uchimbaji.
Mzee Millinga na wenzake walipofika
pale mgodini waliweza kuonana na Watanganyika wengine, waliokuwepo huko na hao
ndiyo waliowapa mbinu za kuwaingia Makaburu na kufanikiwa kupata kazi mgodini.
Hata hivyo hakuridhika na kazi hiyo,
hivyo baada ya miezi miwili aliamua kuondoka pale na kuelekea mjini
Johannesburg na kisha Cape Town ambako alipata ajira, kazi hii ya sasa ilikuwa
ngumu kwa kuwa alipata kazi ya kubeba vifaa vya wachimba migodi, alikuwa
anaingia mgodini asubuhi na kutoka jioni wakati huo malazi yalikuwa katika
hema.
Baada ya mwezi mmoja wafanyakazi
wenzake kutoka Tanganyika walimnong’oneza kuwa kuna nafasi ya kazi ya kitengo
cha Ofisini, wakamsihi aandike barua ya maombi ambapo aliandika barua kuomba
kazi hiyo na katika usaili alifanya vizuri na hapo alifanikiwa kupanda cheo na
kuongezewa marupurupu na kuna wakati alilipwa posho ya ziada kwa kufanya kazi
ya watu wawili.
Mwanzoni mwa mwaka 1950 alirejea
nyumbani Tanganyika baadae alipata habari kuwa baba yake mzazi alikuwa mjini
Dodoma, aliamua kumfuata ili aweze kumshawishi arudi nyumbani Lituhi ambapo
alikubali na akarejea nyumbani, lakini Mzee Millinga hakurudi nyumbani bali
aliendelea na safari hadi Wilayani Ngudu kwa baba yake mdogo aliyekuwa Inspekta
wa Polisi ambapo ilikuwa sasa ni chimbuko la kupata ajira katika Idara ya
Maendeleo ya Jamii, kwa msaada wa rafiki wa Inspekta huyo aliyekuwa anafahamika
kwa jina la Fredrick Mchauro.
Mzee Millinga alijiunga na chama cha
TAA Mkoani Tabora, akiwa mtumishi wa Idara hiyo huko alipandishwa cheo kuwa
katibu wa TAA Tabora katika kipindi hicho, Bwana Mchauro alikuwa amehama Tabora
kabla ya hapo alikuwa Mwenyekiti wa TAA Tabora.
Baada ya safari ndefu ya utumishi wa
Serikali na harakati za TAA na TANU, baada ya Uhuru Mzee huyo akiwa mkazi wa
mtaa wa Lindi na baadae Temeke Wailesi Kota, Dar es Salaam na hapo baada ya
Uhuru alijikita zaidi katika ajira yake ya Serikali.
Utumishi wake ulipitia katika sehemu
tofauti, kuanzia Kilindi alikokuwa amehamia baada ya kutoka Dar es Salaam mara
tu baada ya Uhuru na baadaye alihamia Morogoro na baada ya mizunguko ya muda
mrefu, aliomba ahamishiwe kwao Mbinga ambako aliondoka miaka mingi na kustaafu
utumishi rasmi mwaka 1976.
Mzee Millinga, ambaye ni kati ya
Waasisi 17 wa TANU mwaka 1954 hapa nchini, amefariki dunia usiku wa kuamkia
Machi 5 mwaka 2018 saa 7:40 Mbinga mjini akiwa nyumbani kwake amezungukwa na
familia yake.
Kabla ya kukutwa na umauti afya yake
ilianza kutetereka kuanzia miaka saba iliyopita akisumbuliwa na Kiharusi,
alikuwa akipata matibabu yake katika Hospitali ya Wilaya ya Mbinga, Peramiho
iliyopo Songea na hatimaye alikuwa akitibiwa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Marehemu ameacha Mjane, watoto 10
wakiwemo Wanaume watano na Wanawake watano na kwamba watoto wanne wametangulia
mbele ya haki, pia Marehemu ameacha Wajukuu 29 na Vitukuu 10.
Katika mazishi yake ambayo yameongozwa
na Naibu Askofu wa Jimbo la Mbinga, Padri Josephat Malunda yamefanyika leo
Machi 8 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni, katika makaburi yaliyopo mazingira
ya nyumbani kwake mtaa wa Kihaha Mbinga mjini, viongozi mbalimbali wa Chama na
Serikali waliweza kuhudhuria akiwemo Naibu Katibu Mkuu Taifa wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Rodrick Mpogolo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho na wa
Wilaya ya Mbinga, Beda Hyera.
Hata hivyo kwa upande wa Serikali
alikuwa Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme na Wakurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mbinga vijijini, Gombo Samandito na Mji wa Mbinga, Robert Mageni huku
shughuli hiyo ya mazishi ikiwa imehudhuriwa na Wananchi wengi wa kutoka Mbinga
na nje ya Wilaya hiyo.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi……Amina.
No comments:
Post a Comment