Na Muhidin Amri,
Tunduru.
JUMUIYA ya Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya
ya Tunduru Mkoani Ruvuma imepata Mwenyekiti wake, Zuhura Maftari baada ya
kumchagua kwa ushindi wa kishindo kuongoza jumuiya hiyo.
Msimamizi wa uchaguzi huo ambao
ni wa marudio uliofanyika kwenye ukumbi wa UWT Wilayani humo, ambaye ni Mjumbe
wa Kamati tendaji ya Mkoa huo, Maristela Mapunda akitangaza matokeo ya uchaguzi
huo alisema kuwa Maftari alishinda kwa kupata kura 367.
Alifafanua kuwa katika ushindi huo,
Maftari aliongeza idadi ya kura na kwamba katika uchaguzi uliofanyika hapo awali
wagombea walioshindwa, walikata rufaa huku akiwa na ushindi wa kura 346.
Katika uchaguzi huo jumla ya wajumbe
493 wa jumuiya hiyo walijitokeza kupiga kura, ambapo kura halali zilikuwa 453
na kura 40 ziliharibika.
Alisema kuwa kutokana na matokeo hayo
wagombea wengine, Zainabu Ligola alipata kura 42 ambaye katika uchaguzi huo wa
awali alipata kura 150 hivyo alishuka kwa kura 108.
Mapunda aliwataja Wagombea wengine
kuwa ni, Fatu Hemed Kaisi ambaye katika uchaguzi huo alipata kura 21 akiwa
ameshuka kwa kura 15 ikilinganishwa na kura 36 alizopata katika uchaguzi wa
awali, Sophia Said Mtuchi ambaye alipata kura 18 na kupungukiwa kura 5 ikilinganishwa
na kura 23 alizopata katika uchaguzi wa awali.
Alimtaja mgombea mwingine ni
Asha Alli Mpinga aliyeshika nafasi ya mwisho huku akiwa amepata kura 5 na
kupunguza kura moja ikilinganishwa na kura 6 alizopata katika uchaguzi wa
awali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi
ya wajumbe wa mkutano huo walisema hizo ni salamu tu kwa baadhi ya wanachama
ambao wamekuwa waking’ang’ania kupata madaraka kwa kulazimisha.
Aidha wajumbe hao ambao hawakutaka majina
yao yatajwe walisema kuwa waliwashauri viongozi wao, ambao wamekuwa wakifanya
upendeleo kwa wanachama hao kuheshimu maamuzi ya wajumbe katika mikutano ya
uchaguzi husika na sio vinginevyo.
Awali akisoma kanuni na maelekezo ya
uchaguzi huo, Katibu wa UWT Wilaya ya Tunduru, Mariam Kasembe aliwataka wajumbe
hao kufanya uchaguzi huo kwa kutumia utashi wao na kwamba kufanya uchaguzi kwa
mashinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi, kutawaharibia jumuiya yao.
No comments:
Post a Comment