Dokta Hassan Abbasi. |
Na Mwandishi wetu,
SERIKALI imetenga jumla ya shilingi trilioni 1 kwa mwaka wa
fedha wa 2017/2018 kwa ajili ya kuweza kulipa madeni mbalimbali ya watoa
huduma, wazabuni na watumishi wa umma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) Dokta Hassan Abbasi alisema hayo leo mjini Dodoma, wakati alipokuwa
akizungumza na Waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa miradi na ahadi
mbalimbali za Serikali.
“Kati ya shilingi trilioni 1 zilizotengwa kulipia madeni kwa
mwaka huu wa fedha, shilingi Bilioni 896.3 zimeshalipwa kwa watoa huduma,
wazabuni na watumishi wa Serikali”, alisema Dokta Abbasi.
Alisema hesabu hiyo inajumuisha shilingi Bilioni 43 ambazo
zimelipwa mwezi Februari mwaka huu, ikiwa ni malimbikizo ya wafanyakazi wa
sekta ya umma.
“Madeni mengine ni uhakiki ambao unaendelea na yataendelea
kulipwa siku zijazo na tutawajulisha”, alifafanua Dokta Abbasi.
Vilevile aliongeza kuwa Serikali itawaondolea adha ya usafiri
wananchi wa maziwa makuu likiwemo Ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria.
Kwa upande wa Ziwa Victoria, mkandarasi amepatikana na
majadiliano ya mwisho na kusaini mkataba na kampuni ya STX ya Jamhuri ya Korea
vitafanyika mwezi huu kwa ajili utengenezaji wa meli mpya itakayokuwa na uwezo
wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400.
Kwa upande wa Ziwa Tanganyika zabuni kwa ajili ya
utengenezaji wa meli mpya ya abiria na mizigo itatangazwa mwezi huu.
Meli hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani
400 za mizigo na italeta mapinduzi makubwa katika usafiri ziwani humo.
Kadhalika Dokta Abbasi alieleza kuwa mwezi Julai mwaka huu hapa
nchini watapokea ndege kadhaa mpya ikiwemo Boeing Dreamliner na ukarabati wa
viwanja vya ndege vya Kitaifa, Kimataifa na Kimkoa unaendelea kwa kasi kote
nchini.
No comments:
Post a Comment