Na Muhidin Amri,
Tunduru.
WANAWAKE Wajawazito katika kijiji cha
Tuwe Macho kata ya Tuwe Macho Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, wameishukuru
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Wilayani humo kwa kujenga
Zahanati ambayo hivi sasa inawasaidia kupata tiba na ushauri juu ya masuala ya afya
na uzazi, hivyo kuweza kupunguza idadi ya vifo vya akina mama Wajawajazito kabla
na wakati wa kujifungua.
Walisema kuwa kabla ya TASAF kujenga
Zahanati hiyo, walikuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu na kutumia muda
mwingi kwenda kutafuta huduma husika Hospitali ya Wilaya Tunduru iliyopo mjini hapa,
jambo ambalo liliwafanya kwa kiasi kikubwa kukosa hata muda wa kushiriki kikamilifu
katika shughuli zao za maendeleo.
Aidha wameiomba Serikali kuboresha
mfumo wa utoaji huduma za afya ikiwemo kuwaletea waganga, vitanda vya kujifungulia
sambamba na baadhi ya vifaa tiba ambavyo vitawezesha kupata huduma bora hasa wakati
wa kujifungua.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema
kuwa licha ya Serikali kupitia mfuko huo kujenga Zahanati hiyo katika kijiji
hicho, kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu jirani
na makazi yao bado huduma za afya zimekuwa duni kwa sababu ya ukosefu wa
Daktari na hivi sasa wamekuwa wakimtegemea Mhudumu mmoja tu wa afya.
Zabib Ameir na Hadija Issa walisema Mhudumu
huyo tangu kufunguliwa kwa Zahanati hiyo mwaka mmoja uliopita, amekuwa anafanya
kazi ya kutoa huduma mbalimbali za afya peke yake bila ya Wataalam wa afya,
ambao wangeweza kusaidiana pamoja huku kukiwa na idadi kubwa ya wagonjwa
wanaokwenda kupata matibabu.
Walisema kuwa licha ya TASAF kuonesha
uzalendo na huruma kubwa kwa wakazi wa kijiji cha Tuwe Macho bado changamoto
kubwa waliyonayo sasa ni ya upatikanaji wa baadhi ya huduma kwani Mhudumu
aliyepo hawezi kutoa huduma ambazo zinahitaji mtaalamu ambaye ataweza kufahamu
matatizo ya mgonjwa.
Kwa upande wake Muuguzi pekee
anayefanya kazi katika zahanati hiyo Sada Lusenga, alisema hali ya upatikanaji
wa huduma za afya katika Zahanati hiyo ni nzuri kwani kuna dawa za kutosha na
wananchi wanaendelea kupata matibabu.
Hata hivyo aliongeza kuwa changamoto
kubwa iliyopo ni uhaba wa watumishi kwani aliyekuwa sasa ni mmoja tu, ambapo
ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupeleka watumishi wengine akiwemo
Daktari ambaye ataweza kushirikiana na wenzake katika kuhudumia wagonjwa
ipasavyo.
No comments:
Post a Comment