Na Muhidin Amri,
Madaba.
MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani
Ruvuma, Pololet Mgema amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya
ya Madaba, Shafi Mpenda kuwachukulia hatua za kinidhamu Watumishi wake waliopo
katika Halmashauri hiyo ambao wamehusika na kufanya udanganyifu katika ujenzi
wa vyumba vya madarasa shule ya msingi Kibulang’ombe iliyopo kata ya
Likalangiro Wilayani hapa.
Udanganyifu huo umefanyika kwenye
ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule hiyo na kusababisha ujenzi kusimama
kwa muda kufuatia watu waliopewa dhamana ya kusimamia hilo kukiuka taratibu
husika hasa katika manunuzi vifaa ikiwemo bati geji 32 badala ya geji 30 kama
ilivyoagizwa na Serikali jambo ambalo Mkuu huyo wa Wilaya amesimamisha ujenzi
huo kwa muda mpaka tatizo hilo litakapokwisha.
“Nimewatuma watu wangu kufuatilia kila
mradi unaotekelezwa katika Halmashauri yako, walipofika pale shule ya msingi
Kibulang’ombe kwa kweli ni masikitiko makubwa kwani bati
zilizonunuliwa ni geji 32 badala ya geji 30, kwa hiyo nakuagiza wewe na
wataalamu wako lazima mfuatilie hili ili kujiridhisha ni nani aliyehusika
kufanya udanganyifu”, alisema Mgema.
Katika kata ya Likalangiro alisema
bado kuna miradi mingi haijakwisha ujenzi wake, hivyo ni lazima Viongozi husika
wa Halmashauri wahakikishe wanatafuta fedha kwa ajili ya kuikamilisha ili
wananchi waweze kuitumia kwa faida ya kizazi cha sasa na kile kijacho.
Mgema aliitaja miradi ambayo bado
haijakamilika ni pamoja na madarasa, matundu ya vyoo na majengo ya maabara
huku akisisitiza kuwa wakati umefika kwa uongozi wa Halmashauri ya Madaba kuona
umuhimu wa kutenga pia fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi yote viporo kabla
ya kuendelea na ujenzi wa miradi mipya.
Alisema kuwa katika ulimwengu wa sasa
tunahitaji kuzalisha wasomi wa masomo ya Sayansi ambao watakaokuja hapo baadaye
kufanya kazi katika viwanda vitavyoanzishwa sasa, badala ya kutafuta wataalamu
wengine kutoka nje ya Wilaya hiyo na kuagiza kuanzia sasa kila shule iwe na jengo
la masomo ya Sayansi (maabara) ambalo limekamilika na vifaa vyake vyote vya
masomo darasani ambavyo vitasaidia wanafunzi waweze kusoma vizuri.
Bila kufanya hivyo aliongeza kuwa tutahitaji
wasomi wengi kutoka nchi za nje kama vile Kenya na Uganda kwa ajili ya
kuja kufanya kazi hapa Tanzania katika viwanda vyetu, na kwamba ni lazima sasa
katika Halmashauri hiyo kuhakikisha wanazalisha wasomi wa masaomo ya Sayansi
watakaokuwa msaada katika viwanda vyetu vya hapa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Vastus Mfikwa alikiri uwepo wa miradi kiporo
katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya yake, ambapo alihaidi kuwa katika bajeti
ya mwaka 2018/2019 kipaumbele kilichopo ni kukamilisha miradi yote ambayo
ujenzi na uwekaji wa vifaa husika ndani yake haujakamilika.
No comments:
Post a Comment