Sunday, March 11, 2018

BODABODA MKOA WA RUVUMA WAPEWA ONYO KALI



Na Kassian Nyandindi,  
Songea.

KATIKA kipindi cha mwaka 2017 Mkoani Ruvuma, imeelezwa kuwa jumla ya watu 32 wamefariki dunia na wengine 41 kujeruhiwa vibaya, kutokana na ajali zilizosababishwa na waendesha Pikipiki maarufu kwa jina la Bodaboda.

Vifo hivyo imefafanuliwa kuwa ni ongezeko la vifo 11 vilivyotokea katika kipindi cha mwaka 2016 Mkoani humo.

Gemin Mushy ambaye ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo alisema hayo jana, alipokuwa akitoa taarifa ya ajali za barabarani ambazo zimetokana na waendesha Pikipiki.


Taarifa hiyo alikuwa akiitoa mbele ya Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Ruvuma, ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme.

Mwaka 2017 alisema kuwa ajali hizo ziliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2016 ambazo zilikuwa 21 tu, huku majeruhi wakifikia 99 ambapo haya yote yalitokana na matumizi mabaya ya barabara huku baadhi yao wakikosa sifa ikiwemo kutokuwa na leseni.

Mushy alieleza kuwa madereva wengine walikuwa wakisababisha ajali hizo kutokana na matumizi ya kilevi hasa unywaji wa pombe aina ya Kiroba, huku akiipongeza Serikali kwa kuzuia aina hiyo ya pombe isizalishwe tena hapa nchini kwani ingeweza kuendelea kuleta madhara makubwa katika jamii.

Vilevile aliongeza kuwa katika kundi hilo la waendesha Bodaboda baadhi yao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu kama vile wizi, usafirishaji wa dawa za kulevya, nyara za Serikali na wengine kutumika katika biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Kamanda huyo wa Polisi amewataka waache kujihusisha na vitendo hivyo huku akionya kuwa Jeshi la Polisi litahakikisha kwamba, linachukua hatua kwa wale wote watakaojihusisha na matukio hayo ambayo yanaleta sura mbaya katika jamii na Mkoa kwa ujumla.

Kwa upande wake akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mndeme amewapa onyo kali vijana wanaojihusisha na biashara ya Bodaboda Mkoani humo kukataa kutumika vibaya na baadhi ya watu wenye nia mbaya na nchi yetu, badala yake wahakikishe wanaisaidia Serikali katika suala la ulinzi na usalama na Watanzania waweze kupata fursa ya kuendeleza shughuli zao za uchumi.

No comments: