Hili ni eneo la kata ya Tanga ambalo ujenzi wa Stendi ya kisasa katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma unatarajiwa kuanza kujengwa. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KAMPUNI ya Serikali ya China,
inayoitwa China Sichuan International Cooperation imesaini mkataba wa miezi 18
na Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, kwa ajili ya ujenzi wa Stendi
mpya ya mabasi katika eneo la Tanga kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa hiyo, Mhandisi Samwel Sanya alisema kuwa Mkataba huo unaanzia Machi 25
hadi Septemba 30 mwaka 2019.
Alisema kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni
sita zitatumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa stendi hiyo ya kisasa na
kwamba lengo la kufanya hivyo ni kuendana na kasi ya ukuaji wa mji, hivyo Manispaa
iliamua kutenga eneo la kituo kikuu cha mabasi kuwa katika mtaa huo wa Tanga
ikiwa ni umbali wa takribani kilometa 14 toka mjini Songea.
“Fedha za mradi huu wa stendi zimetolewa
kupitia Benki ya dunia, jumla ya hekari 29 zimetwaliwa katika eneo hilo ili
kupitisha stendi ambapo hekari 20 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 32
tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi”, alisema Sanya.
Kampuni ya China Sichuan International
Cooperation imesaini pia mkataba wa miezi 18 wa ukarabati wa barabara ya lami
nzito katika Manispaa hiyo yenye urefu wa kilometa 10.3 kwa thamani ya zaidi ya
Shilingi Bilioni kumi.
Fedha za miradi hiyo ya barabara na
stendi zimetolewa na Benki ya dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo
Serikali za Mitaa (ULGSP), mpango huo unakusudia kuendeleza miundombinu ya
Halmashauri za miji na Manispaa 18 za Tanzania bara ikiwemo hiyo ya Songea.
No comments:
Post a Comment